Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Takwimu ya Jamhuri ya Korea (KOSTAT) zimekubaliana kushirikiana ili kuimarisha uzalishaji takwimu bora nchini.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Takwimu inaeleza kuwa:
Makubaliano hayo yamefikiwa mwishoni mwa ziara ya siku nne ya ujumbe wa KOSTAT uliokuwa nchini kwa mwaliko wa NBS.
Chini ya makubaliano hayo, KOSTAT inatarajiwa, ndani miaka mitatu kuanzia mwaka kesho, kutoa dola za kimarekani milioni 3 kuisaidia NBS kujenga uwezo wa kiufundi, kitaalamu na miundombinu ya kitakwimu ili kuongeza uwezo wake wa kuzalisha tawimu bora nchini.Akizungumza mwishoni mwa ziara hiyo, kiongozi wa ujumbe huo, Bwana Seong Kido ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Masuala ya Takwimu alisema ujumbe wake umevutiwa na namna NBS inavyotekeleza makujumu ya kuzalisha takwimu.“Tanzania ni nchi kubwa lakini kiidadi ya watu karibu tuko sawa (Jamhuri ya Korea). Taasisi yetu ina watumishi wapatao 3,000; nyinyi mko kidogo lakini mnaweza kuzalisha takwimu nyingi” Alisema bwana Kido na kuongeza kuwa NBS inajitihadi sana.Alisema ziara yao nchini imekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa imefungua milango kwa KOSTAT kufanya kazi kwa karibu na NBS.“Tumekuja NBS tukiwa na dhamira ya kuanzisha ushirikiano kati ya taasisi zetu kwa kuangalia mazingira na pia kuangalia maeneo ambayo tunaweza kufanyakazi pamoja na kuanzisha ushirikiano wa muda mrefu kwa manufaa ya nchi zetu na hili linawezeka”alisema Mkurugenzi huyo.Naye Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Shughuli za Kitakwimu wa NBS Irenius Ruyobya, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NBS aliushukuru ujumbe huo kwa namna walivyoshirikiana na NBS wakati wote walipokuwa nchini.“Tunawashukuru kwa namna mlivyoshirikiana nasi wakati wote mlipokuwa hapa jambo ambalo linadhihirisha utayari wa KOSTAT kufanya kazi kwa karibu na ofisi yetu”alisema Ruyobya na kusisitiza kuwa ziara hiyo ni mwanzo wa safari ndefu ya ushirikiano wa dhati kati ya NBS na KOSTAT.Wakati huo huo, akiukaribisha ujumbe huo ofini kwake barabara ya Kivukoni jijini, Mkurugenzi Mkuu wa NBS Dkt. Albina Chuwa alieleza kuwa NBS imefurahishwa sana ujio wa ujumbe ambao dhamira yake kubwa ni kuanzisha ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili.“Tuna furaha kuwakaribisha Tanzania na hasa hapa NBS. Naamini ushirikiano kati ya taasisi zetu ni matunda ya uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi zetu mbili” Dkt. Chuwa alieleza.Aliongeza kuwa anaamini kuwa NBS ina mengi ya kujifunza kutoka KOSTAT hivyo ushirikiano kati ya taasisi yake na taasisi hiyo ni muhimu kwa kuwa anaamini utachangia uwezo wa Tanzania kuzalisha takwimu bora.Ukiwa NBS ujumbe huo ulipata fursa ya kutembelea Idara mbali mbali na kufanya majadiliano na watumishi wa Idara hizo zikiwemo Idara ya shughuli za kitakwimu, Idara ya Sensa wa Watu na Makazi, Idara ya Takwimu za Kijamii, Idara ya Tehama na Idara ya Mifumo ya Taarifa za Kijiografia. Ujumbe huo ulitembelea pia ofisi za NBS mkoa wa Pwani, zilizopo Kibaha.
Post A Comment: