Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema takribani wafanyakazi 20 akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Wanawake Magreth Chacha, wanachunguzwa na Takukuru kutokana na kukosa uadilifu na kuisababishia hasara benki hiyo.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu katika mkutano wa 10 kikao cha sita cha Bunge kinachoendelea mjini Dodoma wakati alipokuwa akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mbunge wa viti maalumu (CCM), Faida Mohamed Bakari aliyetaka kufahamu ni hatua zipi zimechukuliwa za kisheria dhidi ya uongozi na watumishi wa benki ya wanawake wasiokuwa waadilifu.
"Kuna mambo yamefanyika ya hovyo unakuta kuna saccos inakopeshwa Bilioni moja, tunaifuatilia hiyo saccos haionekani hizo fedha zimekwenda kwa nani. Kwa hiyo nataka kumuhakikishia Mhe. Faida kwamba tunaamini PCCB na Polisi watakamilisha uchunguzi haraka na lengo letu hawa watumishi hawakuwa waaminifu waweze kwenda mbele ya vyombo vya dola na kuchukuliwa hatua dhidi yao", amesema Ummy.
Kwa upande mwingine, Mhe.Ummy amesema serikali imedhamiria kuhakikisha wanapata fedha ya kukuza mtaji wa benki ambapo wamepewa miezi sita na benki kuu ya Tanzania (BoT).
Post A Comment: