SERIKALI imeendelea kudhibiti ubora wa elimu nchini kwa kuvichukulia hatua vyuo na shule zinazobainika kukiuka taratibu za utoaji wa elimu ikiwa ni pamoja na kusitisha udahili wa wanafunzi,kusitisha program zitolewazo,kupunguza idadi ya wanafunzi waliozidi na kufuta usajili wa taasisi husika.
Aidha katika Mwaka 2017/18 ulifanyika uhakiki katika vyuo na taasisi 458 za elimu ya ufundi ambapo jumla ya vyuo na taasisi 59 zilibainika kuwa na mapungufu na hivyo walitakiwa kurekebisha mapungufu hayo ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia Februari 1 Mwaka 2018,chuo kitakachoshindwa kurekebisha mapungufu hayo kitafutiwa usajili.
Kauli hiyo imetolewa leo bungeni na Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,William OleNasha alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum,Zubeda Sakuru (Chadema),lililoulizwa kwa niaba yake na Mbunge wa Viti Maalum,Susan Lymo,.
Katika swali hilo ambalo lilihoji “Baadhi ya shule na vyuo nchini vinaendelea kudahili wanafunzi pamoja na kutokidhi matakwa ya sheria mbalimbali,Je serikali inachukua hatua gani kudhibiti vyuo na shule zinazoendelea kudahili wanafunzi huku zikiwa na mapungufu,Je hadi sasa ni vyuo na shule ngapi zilizofutiwa usajili kwa kutokidhi matakwa ya kisheria?”
Akifafanua katika majibu yake OleNasha alisema kwa upande wa vyuo vikuu serikali kupitia TCU ilifanya uhakiki wa Vyuo vyote vya Elimu ya juu nchini kati ya Ocktoba 2016 na Januari 2017 ili kuhakiki ubora wa elimu inayotolewa vyuoni .
“Taarifa ya uhakiki inaonesha mapungufu katika baadhi ya vyuo ,kufuatia programu hiyo TCU kwa Mwaka wa masomo 2017/18 ilisitisha udahili wa wanafunzi wa programu za Afya na uhandisi kwenye vyuo vitano’’alisema OleNasha na kuongeza kuwa
“Vilevile,TCU ilisitisha udahili katika program zote kwa Mwaka wa kwanza wa vyuo 14 ,katika Mwaka huo huo wa masomo TCU imedhibiti na kuzuia vyuo vikuu kudahili wanafunzi katika program ambazo hazijapata ithibati zipatazo 75 katika vyuo vikuu 22’’
Post A Comment: