Mchezaji wa kimataifa wa Tanzania Mbwana Ally Samatta akiwa na klabu yake ya KRC Genk amefanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Ubelgiji baada ya kushinda mchezo wa nusu fainali dhidi ya Kortrijk.
Katika mchezo huo uliopigwa usiku wa kuamkia leo Samatta amecheza dakika zote 90 na kuisaidia timu yake kushinda bao 1-0 katika nusu fainali ya pili hivyo kufanya matokeo ya jumla kuwa 3-3 na Genk kufuzu kwa faida ya goli la ugenini baada ya Genk kupoteza 3-2 kwenye nusu fainali ya kwanza.
Bao pekee la Genk limefungwa na kiungo Ibrahima Seck ambaye ni raia wa Senegali katika dakika ya 15 akimalizia pasi ya Mhispania Alejandro Pozuelo Melero.
Katika mchezo wa fainali, Genk inasubiri kujua mpinzani wake ambaye atashinda kwenye nusu fainali ya pili kesho kati ya timu za Club Brugge na Standard Liege. Matokeo katika mchezo wa kwanza Liege wanaongoza kwa mabao 4-1.
Samatta jana amecheza mechi yake ya nne tangu apone majeraha ya goti yaliyomweka nje kwa miezi kadhaa. Nahodha huyo wa Taifa Stars pia amefikisha michezo 74 ndani ya klabu hiyo ambayo alijiunga nayo Januari 2016.
Post A Comment: