Wakimbizi watano kutoka DR Congo wameuawa katika maandamano yaliofanyika Jumanne nchini Rwanda yakipinga uamuzi uliochukuliwa wa kupunguziwa ruzuku waliyokuwa wakipewa na Shirika la UNHCR.
Jeshi la Polisi la Rwanda limethibitisha taarifa hiyo Ijumaa hii Februari 23, 2018 na kusema kuwa kuna wakimbizi wengine 20 wamejeruhiwa kwenye maandamano hayo.
Kwa mujibu wa msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Rwanda, Theos Badege kwenye mahojiano yake na kituo cha Shirika la Habari la Anadolu, amesema wakimbizi waliojeruhiwa walikuwa wakitumia nguvu katika maandamano.
Jeshi la Polisi lililazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji hao, ambapo baadhi ya waandamanaji walikuwa na visu huku ikiripotiwa kuwa polisi 7 walijeruhiwa.
Maandamano hayo yalifanyika mbele ya ofisi za kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachohudumia wakimbizi UNHCR, Mjini Karongi Magharibi mwa Rwanda ambapo zaidi ya Wakimbizi 3,000 waliandamana.
Kwa upande mwingine, Mwakilishi wa wakimbizi katika kambi hiyo, Jean-Louis ameomba kuhamishwa kwa wakimbizi nchini Rwanda akidai kuwa hawatendewi haki na kudhulumiwa.
Tayari Shirika linaloshughulikia Wakimbizi duniani (UNHCR) limelaani mauaji hayo huku likitaka uchunguzi ufanyike haraka kujua chanzo cha migogoro kwenye kambi hiyo.
Post A Comment: