Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amewaagiza wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite kuwalipa mishahara wachimbaji na wasipotimiza hilo wasitishe shughuli hizo.
Mnyeti amesema hayo leo Februari 25,2018 alipozungumza na wamiliki wa migodi, mameneja na wachimbaji katika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro.
Amesema utekelezaji wa agizo lake unapaswa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.
Mkuu huyo wa mkoa amesema hakuna mjadala katika utekelezaji kwa kuwa kwa muda mrefu wamiliki wa migodi wanajinufaisha wao na familia zao bila kujali haki za wachimbaji.
Mmoja wa wamiliki wa migodi, Abubakary Madiwa amesema suala la kuwalipa mishahara wachimbaji litakuwa gumu kutekelezwa.

Madiwa amesema endapo hilo litafanyika ni wamiliki wapatao 10  watakaokuwa na uwezo wa kulipa mishahara wafanyakazi wao.
"Ni bora ungesema migodi ifungwe kuliko kutuagiza tuwalipe mishahara wachimbaji hawa kwa kuwa tuna utaratibu wa kuangalia haki zao pindi uzalishaji unapofanyika," amesema Madiwa.
Mnyeti akijibu hoja ya Madiwa amesema, "Kama wewe huwezi kulipa mishahara ya wafanyakazi wa migodini ufungashe virago urudi nyumbani, ukatafute kazi nyingine ya kufanya,"
"Sheria haina huruma, mama mjane au mwanamke ni kule nyumbani huku machimboni anakuwa mkurugenzi wa mgodi, sina huruma kwa hilo walipeni mishahara wafanyakazi wenu," amesema
Kaimu katibu tawala mkoa, Missaile Mussa amesema wachimbaji wa madini wanapaswa kulipwa mishahara kwa mujibu wa sheria ya kazi namba sita ya mwaka 2004.
Mussa amesema wachimbaji wanastahili kupatiwa mishahara na stahili zao kama wafanyakazi wengine.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: