Wananchi hao walikuwa wakiandamana kushangilia kuachiwa kwa mwenyekiti wao wa kijiji cha Ngarenairobi (Chadema), Stanley Nkini, mara baada ya mahakama kumwachia kwa dhamana.
Maandamano hayo yaliyoonekana kuwa ni ya amani hadi polisi walipoingilia kati na kuwatawanya waandamanaji kwa mabomu ya machozi, yalitokea kati ya saa 10:00 na saa 11:00 jioni.
Mwenyekiti huyo na wenzake wawili ambao ni Peter Munuo na Thomas Mollel, walikamatwa na polisi na kufikishwa kortini katika mahakama ya Siha leo Februari 6 kwa kosa la wizi wa kutumia nguvu na shambulio.
Mbele ya Hakimu Mkazi wa wilaya ya Siha, Doroth Mateni, ilidaiwa kuwa Februari 4, walimwibia mwenyekiti wa kitongoji cha Mwangaza (CCM), Emil Ndesamburo, simu ya mkononi na Sh180,000.
Mara baada ya kusomwa kwa mashitaka hayo, washitakiwa hao waliyakana na hakimu kuwaachia kwa dhamana, hali iliyoibua furaha kwa baadhi wananchi waliokuwa wamefurika mahakamani hapo.
Kaimu Kamanda wa polisi Mkoani Kilimanjaro, Koka Moita, amesema walitumia mabomu hayo kuwatawanya wananchi hao kwa vile maandamano hayo yalitaka kuleta uvunjifu wa amani.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda huyo, katika kuzima maandamano hayo kwa kutumia mabomu ya machozi, polisi walifanikiwa kurejesha hali ya amani na hakuna mtu aliyejeruhiwa au kupigwa.
Wilaya ya Siha kwa sasa inashuhudia kampeni nzito za uchaguzi mdogo wa Ubunge Jimbo la Siha, ambapo mchuano mkali zaidi umekuwa baina ya vyama viwili ambavyo ni Chadema na CCM.
Chadema kimemsimamisha Elvis Mosi, wakati CCM kimemsimamisha Dk Godwin Mollel aliyekuwa mbunge wa Jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema, kabla ya kujiuzulu mwaka jana na kujiunga na CCM.
Baadaye vikao vya juu vya CCM chini ya mwenyekiti wake, Rais John Magufuli, viliamua kumteua Dk. Mollel kupeperusha bendera ya chama hicho kuchuana na vyama vitatu vilivyosimamisha wagombea.
Post A Comment: