Related image

Zaidi ya wakulima 30,000 kutoka skimu 11 za umwagiliaji wa mpunga wilayani Iringa watanufaika na mradi wa kuzuia upotevu wa mpunga baada ya mavuno na kuongezewa mnyororo wa thamani.

Mradi huo unatekelezwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).
 Akizungumza kwenye mkutano wa uzinduzi huo Mwakilishi Mkazi wa FAO, nchini Fred Kafero, alisema mradi huo unalenga kuwaunganisha wakulima, wasindikaji na wanunuzi kwa mafunzo na  mashine za usindikaji wa kuongeza thamani.

Kafero alisema ufikiwaji wa masoko yenye faida lazima uboreshwe, ili wakulima wafaidike na juhudi zao huku Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela, akisema  wana uhakika utawaongezea kipato pamoja na soko la uhakika.

Tarafa za Pawaga na Idodi ndizo zinazozalisha mpunga kwa wingi, lakini taarifa zinaonyesha asilimia 15 hadi 40 ya mpunga unaozalishwa hupotea kabla ya kufika sokoni kutokana na mbinu duni za uhifadhi.

Mradi huo unaofadhiliwa na Muungano wa Ulaya (EU) kwa thamani ya Sh.  bilioni 5.2  na utawawezesha wakulima wa mpunga mkoani Iringa kuhimili ushindani wa soko na kukabiliana na changamoto za upotevu wa mazao yao.

Meneja wa mradi kutoka EU), Liesl Inglis, alisema:  “Mradi tunaoizundua leo ni moja ya miradi mitatu ambayo inafadhiliwa na EU, nashukuru  kwa sababu mwakilishi kutoka wizara ya fedha ameishaitaja miradi ambayo inatekelezwa na mikoa ya Morogoro na Iringa.”
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, aliwataka watendaji wa vijiji kusimamia skimu za umwagiliaji zidhibiti wizi wa fedha za wanachama wao.

Masenza aliomba ufadhili huo kuona jinsi ya kuwasaidia kwa kuwafungia mashine,  ili walime, wavune, kufungasha pamoja na kukoboa kwa jina la Pawaga au Idodi kwa lengo la kuutangaza mkoa wa Iringa.

Alisema tatizo la upotevu na uharibifu wa zao hilo ni kubwa kutokana na mbinu duni za uvunaji, ukaushaji, usafirishaji, uhifadhi na usindikaji.
Baadhi ya wakulima Fredrick Funzila na Oswald Kapungu walisema  wakati wanavuna mpunga wanatakiwa pia kuvuna mahindi na hicho ndicho kinachowafanya kupoteza baadhi ya mazao huku.

 Kapunga alisema wanahifadhi mpunga kwenye maeneo ambayo hayastahili, ikiwamo kushambuliwa na wadudu au panya.
Share To:

Post A Comment: