Akizungumza leo Februari 3, 2018 katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Sekondari ya Mama Salma Kikwete, Mtulia amesema atatoa magari hayo kwa kuwa anajua matatizo ya wakazi wa Kinondoni.
Amesema tatizo kubwa la Kinondoni ni kuwa na takataka maeneo mengi, kusisitiza kwamba magari hayo yatasaidia kupunguza takataka na kupunguza ajira.
“Jana niliahidi kutoa Sh10 milioni kwa saccos ya Kigogo na nyinyi nawaambia mkiunda Saccos mje kwa mbunge kuchukua fedha yenu ipo,” amesema.
Mtulia alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CUF kuanzia mwaka 2015, Desemba 2017 alihamia CCM ambako alipitishwa tena kuwania ubunge.
Pia amezungumzia gharama za kuhifadhi maiti mochari, “Hili nalituma kwa mheshimiwa Rais, haliko ndani ya uwezo wangu, naomba alisikilize ningependa wananchi wa Kinondoni wahifadhi miili ya wapendwa wao hospitali bila kulipa chochote.”
“Tutawaonyesha wenzetu wa upinzani nini kinatakiwa kufanywa kwa wananchi badala ya maneno mengi.”
Akizungumza katika mkutano huo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Uhusiano wa Kimataifa, Kanali mstaafu, Ngemela Lubinga amesema, “Tumeshatenga Sh70 milioni kwa ajili ya ujenzi wa vyoo vya stendi ya Mwenge. Mchagueni Mtulia asimamie kazi zenu ikiwamo kutumia vema fedha za wilaya ya Kinondoni ikiwamo Sh40 milioni za ukarabati wa shule ya Mama Salma Kikwete.”
Amesema uhakika wa maendeleo ya vijana sambamba na maisha yao chini ya CCM ni mkubwa.
“Mpeni kura Mtulia akasimamie Sh45 milioni za mikopo ya kina mama na vijana. Najua mlikuwa mnacheleweshewa, lakini kwa hili jembe sina shaka mtapata kama inavyostahili,” amesema.
Naye mgombea wa Chadema, Salum Mwalimu akizungumza katika mkutano uliofanyika Hananasif, amesema, “Mkinichagua hii biashara ya kuvunja nyumba za watu bila taarifa za kutosha na fidia itakuwa mwisho nakwenda kushughulika na hilo.
Nazungumza kwa uchungu kwa kuwa naelewa matatizo ya wakazi wa Hananasif nami nyumba yangu inaweza kubomolewa.”
Akimnadi Mwalimu, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji amesema, “Huu uchaguzi ni mkakati wa makusudi wa kuficha ukweli. Wanataka kuonyesha kwamba kuna mtu fulani anapendwa zaidi na watu wanamuunga mkono.”
“Kumweka Salum Mwalimu haikuwa bahati mbaya, anajua fika tumekuwa tukiandika mikakati mingi ndani ya chama ambayo inasimamia ajira na kipato.”
Dk Mashinji pia amegusia kauli ya Rais John Magufuli ya kuwashangaa majaji kusafiri nje ya nchi wakati kiwango chao cha mishahara anakifahamu, “Kwanini hashangai watumishi wa umma wanaolipwa kiasi kidogo cha mshahara wanavyomudu gharama za maisha ambazo ni kubwa kuliko uwezo wao.
Post A Comment: