NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete swali la nyongeza
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE:Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Waziri nafikiri leo unatambua kwamba leo ndio tarehe ya mwisho ya ule mradi maji Chalinze, ninachotaka hapa ni kusikia kauli ya Serikali juu ya nini sasa kinafuata baada ya leo kuwa deadline ya ule mkataba wetu wa ujenzi wa mradi wa maji Chalinze?
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji majibu.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge Kikwete kama ifuatavyo:-
Kauli hiyo unayoizungumza iko katika taratibu za kimikataba, nikishauri tu Mheshimiwa Mbunge sisi wanasiasa watunga sera si vyema tuingilie mikataba, tusubiri kwanza utekelezaji wa mikataba ufanyike hatua zitakazochukuliwa basi tutazitolea taarifa.
Time: 11.22 - 11:25 am
MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Ridhiwan Kikwete
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Nasimama kwa Kanuni ya 68(7) nikiomba Mwongozo wako mapema leo niliposimama kuuliza swali la nyongeza kufuatia swali lililoulizwa na dada Lathifah, majibu niliyopewa na Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa kweli binafsi yangu hayakunifurahisha kabisa, nataka niliweke wazi hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimetumwa na watu wa Chalinze, kwa maana Jimbo la Chalinze, Halmashauri ya Chalinze kuja kuuliza juu ya shida zao, sifanyi siasa katika jambo hili. Ninatambua kwamba mkataba wa maji baina ya Mamlaka yetu pale kwa maana ya CHALIWASA, DAWASCO na Wizara kwa maana ya Serikali na yule mkandarasi inakwisha leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninajua hilo, nauliza Serikali inipe juu ya nini kinafuatia baada ya mkataba huo kuisha, majibu ninayopewa na Waziri yanaonekana kama mimi nafanya siasa katika jambo la kitaalam. Nataka nimkumbushe Mheshimiwa Waziri kwanza mimi ni mwanasheria, ninaelewa ninachokifanya na nimetumwa na watu walio na akili timamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia hapo hapo nataka nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, ninaposimama leo hii hapa, huu ni mwezi wa pili sasa unakwenda wa tatu wananchi wanaoishi katika Halmashauri ya Chalinze hawapati maji kabisa. Sasa leo hii nasimama hapa unanijibu kwamba mimi nataka nifanye siasa, Mheshimiwa Waziri hata kama tulichaguliwa kwa siasa lakini mimi sifanyi siasa, naomba nikupe taarifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu hii inafanya juhudi kubwa kuendeleza viwanda na Chalinze inafahamika kwamba ndio sehemu yenye chemchem ya viwanda kwa sasa, lakini cha kushangaza kukosekana kwa maji kumepelekea Kiwanda cha Sayona kufungwa, natoa taarifa hiyo hapa, kiwanda kimefungwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi ninaposimama na ninapouliza nini kauli ya Serikali juu ya way forward baada ya mkataba huu kuisha siku ya leo, najibiwa majibu ambayo yanakatisha tamaa sio kwangu mimi tu, lakini hata Rais wangu Mheshimiwa John Pombe Magufuli naye pia hayapendi majibu hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba, naomba Mwongozo wako juu ya kauli ya Serikali, juu ya nini kinafuatia baada ya mkataba huu kufa leo lakini nini ambacho kinatakiwa kifanyike ili kuhakikisha kwamba sera iliyowekwa na CCM, sera iliyosimamiwa na Serikali yetu, inayosimamiwa na mimi Mbunge na maendeleo ya Chalinze na wananchi wangu wa Chalinze wanaohangaika kutafuta maji wakati maji tunayo, mradi upo lakini hatuelewi kinachofanyika…
MWENYEKITI: Umeeleweka Mheshimiwa Kikwete.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Post A Comment: