Mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki kwa tiketi ya chama cha demokrasia na maendeleo Chadema Mh Joshua Nasari leo amefikishwa mbele ya hakimu wa mahakama ya Arumeru iliyopo kata ya Sekei na kusomewa shitaka moja la shambulio .
Akisoma shitaka hilo wakili wa serikali Fortunatus Muhalila mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Jasmin Abdul, alisema kuwa Mbunge Nasari anakabiliwa na shitaka moja la shambulio ambalo alitenda desembe 14 mwaka 2014.
Wakili wa serikali aliendelea kusema kuwa Nasari alimshambulia, Neemani Ngudu mkazi wa kata ya Makiba kwa kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia maumivu makali kitu ambacho Joshua Nasari alikataa shitaka hilo.
Mara baada ya wakili wa serikali kumaliza kusoma shitaka hilo na mtumiwa kukataa kutenda kosa hilo ndipo Hakimu Jasmini Abduli aliamua kusema dhamana ipo wazi na mdhamini mmoja mwenye barua ya utambulisho na kusaini dhamana yenye thamani ya shilingi milioni tano kitu ambacho mbunge huyo alitimiza masharti na kuachiwa huru kwa dhamana.
Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi machi 3 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena, huku wakili mtetezi wa upande wa Nasari unasimamiwa na wakili msomi Sheck Mfinanga.
Awali hapo jana Mbunge Nasari alifika katika kituo cha polisi Usa River lengo likiwa ni kufuatilia silaha yake aina ya bunduki inayoshikiliwa katika kituo hicho lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida alifahamishwa kwamba anakabiliwa na kosa la shambulio lililotendeka mwaka 2014 na hivyo kutakiwa kifika mahakamani kesho yake yaani leo siku ya jumanne ,feb 6 mwaka 2018 kwa ajili ya kusomewa shitaka lake ili aweze kujibu.
Post A Comment: