Anasema teknolojia ya kubebesha miche ya mikorosho kwake imekuwa mkombozi kwa kumwongezea mavuno na kwamba sasa amepata nguvu ya kuondoa miche ya asili katika shamba lake.
“Nilipata teknolojia hii ya kubebesha miche kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Naliendele mkoani Mtwara.
Mikorosho ya kisasa
“Nimeamua kuboresha shamba langu kwa kupanda mikorosho ambayo inatokana na teknolojia ya kubebesha miche, ukiangalia hapa shambani utaona kuna miche midogo ipo karibu na mikubwa, hapa nina maana kuwa mche huu mdogo utakapoanza kutoa mavuno mengi, huu mkubwa nauondoa,” anabainisha Namwete.
Mkulima wa Korosho wa Kijiji cha Kitama wilayani Tandahimba, Hamis Kitemwe anasema teknolojia ya kubebesha miche ya mikorosho imekuwa chachu ya ongezeko la uzalishaji wa korosho kwa wakulima katika wilaya hiyo.
“Ukiangalia shamba langu utagundua mikorosho mingi ni michanga, hii ni ile ambayo imebebeshwa, mikorosho hii inazaa sana, inavumilia magonjwa na inatoa korosho bora,” anabainisha Kitemwe.
Kaimu Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Tandahimba, mkoani Mtwara, Mohamedi Majogo anasema moja ya sababu ya wilaya yake kuongoza kwa kuzalisha korosho nchini ni pamoja na wakulima kupokea vizuri teknolojia za kuzalisha zao hilo zinazotolewa na Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Naliendele ikiwa pamoja na teknolojia ya kubebesha miche ya mikorosho.
“Wakulima wangu wameipokea teknolojia ya kubebesha miche mikorosho, mikorosho mingi ni ile iliyotokana na teknolojia hiyo, msimu wa kilimo 2012/13 tumezalisha zaidi ya tani 34,985 za korosho, ingawa kiwango hicho ni pungufu ukilinganisha na msimu uliopita ambao tulivuna tani 47,000 bado teknolojia ya kubebesha inaonyesha mafanikio makubwa.
“Katika wilaya yangu wapo wakulima wanafahamu kanuni za kilimo bora cha Korosho kuliko maofisa kilimo, hii inaonyesha jinsi gani wakulima wangu walivyopokea vizuri teknolojia ya kuzalisha zao hili,” anasema Majogo
Mtafiti wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Naliendele, Ramadhani Bashiru anasema teknolojia hiyo ni utaratibu wa kuridhisha vinasaba kutoka kwenye mti mama kwenda kwenye shina.
Anasema teknolojia hiyo inalenga kuhamisha tabia nzuri za mkorosho mama na kupandikiza kwenye shina lingine kwa lengo la kupata matokeo ya mti mama.
“Ubebeshaji ni kitendo cha kuunganisha miti miwili ya jamii moja au tofauti ili iweze kukua na kuendelea kuishi kama mti mmoja, kunakuwapo mti unaochangia mizizi (shina) na mti unaochangia matawi (kikonyo).
“Tunahamisha tabia nzuri za mkorosho mama na kuzipandikiza kwenye shina lingine, mkorosho uliobebeshwa utakuwa na tabia kama zile za mkorosho mama, tunachukua vikonyo vya mkorosho mama na tunakwenda kubebesha kwenye shina la mche mchanga au mkongwe,” anaeleza Bashiru.
Anafafanua kwamba teknolojia hiyo inaziba nafasi ya kupanda mbegu ambazo licha ya kuchukua muda mrefu hadi kupata mavuno, lakini pia mkorosho unaweza kuwa na tabia tofauti na za mkorosho mama.
“Ukipanda mbegu hakuna uhakika kwamba tabia za mkorosho mama zinaweza kurithishwa kwenye mmea mpya bali kupitia hii teknolojia ya ubebeshaji kuna uhakika wa asilimia 100 ya tabia nzuri za mkorosho mama kurithiwa na mmea mpya.
“Mkorosho iliyobebeshwa inaweza kuanzaa kuzaa ndani ya mwaka mmoja, tofauti na ukipanda mbegu ambayo itachukua miaka mitatu hadi mitano,” anasema.
Faida ya teknolojia
Anabainisha kwamba mkorosho uliobebeshwa una faida nyingi zikiwamo uhakika wa mavuno mengi, uvumilivu wa magonjwa na ubora wa korosho zenyewe.
“Kuanzia mwaka wa kwanza unaanza kuvuna, ila kitaalamu tunashauri maua ya mwaka wa kwanza yaondolewe kwa sababu mmea utakuwa hauwezi kubeba matunda. Kadri umri wa mkorosho unavyokuwa ndivyo mavuno yanavyoongezeka,” anaeleza Mtafiti huyo .
Anasema changamoto kubwa katika kufanikisha teknolojia hiyo ni upatikanaji wa ubebeshaji bora wenye uwezo wa kutoa asilimia 80 ya miche itakayokuwa vizuri.
“Unaweza kubebesha ndani ya mwaka mzima ila tunashauri kwamba Mei hadi Julai sio wakati mzuri kwa sababu vikonyo vinakuwa vimejiandaa kutoa maua, ukibebesha wakati huu kikonyo kinaweza kutoa maua abadala ya majani.
“Oktoba hadi Novemba nao si muda mzuri , kwa sababu wakati huu unakuwa wa kiangazi sana, vikonyo vinakosa maji ya kutosha kuchipua, muda mzuri tunaopendekeza ni mwishoni mwa Novemba hadi Machi kwa sababu wakati huu, mikorosho itakuwa imepata maji ya kutosha na inajiandaa kuchipua, inakuwa katika kipindi cha ubwete (dormancy),” anabainisha Bashiru.
Anasema baada ya kuandaa miche hiyo wanaisambaza kwa wakulima ikiwa ni sehemu ya kusambaza teknolojia kwa wakulima .
“Tulitaka teknolojia hii imilikiwe na wakulima wenyewe, hivyo tumefundisha wakulima, karibu kila wilaya ambako korosho zinazalishwa.
“Maeneo kama ya Tandahimba hakuna shaka kwamba wamepokea teknolojia hii vizuri, ndiyo maana uzalishaji uko juu kuliko eneo lolote hapa nchini,” anasema.
Post A Comment: