Serikali ya Marekani imesema kuwa imesikitishwa na hatua ya kiongozi wa upinznai nchini Kenya Raila Odinga ya kujiapisha Jumanne wiki hii.
Aidha katika hatua nyingine, Marekani imeituhumu serikali hiyo kwa kufungia vituo vinne vya habari nchini humo ambavyo viliadhibiwa baada ya kurusha matangazo ya moja kwa moja hafla ya uapisho wa kiongozi huyo wa upinzani.
Taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema kuwa taifa hilo linaamini mizozo yoyote ile inafaa kutatuliwa kwa njia stahiki za kisheria.
“Tunakataa vitendo vyovyote ambavyo vinahujumu Katiba ya Kenya na utawala wa sheria. Uhuru Kenyatta alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya Oktoba 26, 2017 katika uchaguzi ambao uliidhinishwa na Mahakama ya Juu,” taarifa hiyo iliyotumwa na msemaji wa wizara hiyo Hearther Nauerth imesema.
Hata hivyo, Marekani imewahimiza viongozi wa kisiasa nchini Kenya kufanya mazungumzo kwa lengo la kuimarisha uwiano na utengamano na kutatua matatizo ya muda mrefu nchini humo
Post A Comment: