Mshambuliaji wa klabu ya soka ya Simba SC, John Bocco ameelezwa kupona majeraha aliyoyapata kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mwadui FC na muda wowote ataanza kucheza kama kocha atampanga.
Afisa habari wa Simba Haji Manara amethibitisha hilo wakati akijibu maswali ya mashabiki wa klabu hiyo waliokuwa wanataka kujua hali ya nahodha huyo wa Simba kupitia ukurasa wake wa Instagram.
''Niwajuze tu kuwa hali ya Bocco anaendelea vizuri na yupo tayari kucheza kama kocha atampanga'', Manara alimjibu moja ya mashabiki waliouliza.
Aidha Manara ameongeza kuwa majeruhi pekee aliyebaki kwenye kikosi cha Simba ni Haruna Niyonzima ambaye hivi karibuni alipelekwa India kwaajili ya matibabu na Manara ameongeza kuwa naye yupo mbioni kurejea.
Majeruhi wengine wa muda mrefu ndani ya kikosi cha Simba ambao tayari wameanza mazoezi mepesi ni mlinda mlango Said Nduda na mlinzi Salim Mbonde ambao wote wamesajiliwa msimu huu wakitokea Mtibwa Sugar.
Post A Comment: