Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ameikosoa kauli ya Mkuu wa Mkoa Alexander Mnyeti kuhusu kuwataka wamiliki ya migodi ya Tanzanite kuwalipa mishahara wachimbaji na endapo watashindwa kutekeleza hilo basi wakusanye virago vyao.
Mh. Lema amesema kwamba kaiuli hiyo ya Mkuu wa Mkoa huenda itaweza kuua biashara ya Tanzanine na badala yake ameshauri ufanyike utafiti wa kina ni pamoja na kuitaka wizara husika kutafuta njia sahihi yenye faida kwa pande zote mbili.
Leo mapema RC Mnyeti alipokuwa akizungumza na wamiliki wa migodi, mameneja na wachimbaji katika mji mdogo wa Mererani wilayani Simanjiro amesema utekelezaji wa agizo lake unapaswa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.
Mkuu huyo wa mkoa amesema hakuna mjadala katika utekelezaji kwa kuwa kwa muda mrefu wamiliki wa migodi wamekuwa wakijinufaisha wao na familia zao bila kujali haki za wachimbaji.
Aidha RC Mnyeti amenukuliwa akisema "Kama wewe huwezi kulipa mishahara ya wafanyakazi wa migodini ufungashe virago urudi nyumbani, ukatafute kazi nyingine ya kufanya,"
Ameongeza "Sheria haina huruma, mama mjane au mwanamke ni kule nyumbani huku machimboni anakuwa mkurugenzi wa mgodi, sina huruma kwa hilo walipeni mishahara wafanyakazi wenu,".
Naye Kaimu Katibu Tawala Mkoa, Missaile Mussa amesema wachimbaji wa madini wanapaswa kulipwa mishahara kwa mujibu wa sheria ya kazi namba sita ya mwaka 2004
Post A Comment: