Kocha Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Aristica Cioaba, ameweka wazi kuwa kikosi hakitarudi nyuma kwenye mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) badala yake amekipanga kukirejesha kileleni.
Mara baada ya Azam FC kupoteza wikiendi iliyopita dhidi ya Yanga, kumekuwa na maneno mengi kutoka kwa mashabiki wengi wa soka wakidai kuwa kipigo hiko kitaishusha timu hiyo na kumaliza mbio za kuwania ubingwa wa ligi.
Lakini Azam FC ikarejea vema kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) jana Jumanne baada ya kusonga mbele kwa hatua ya 16 bora ikiichapa vilivyo Shupavu ya Morogoro mabao 5-0, huku mshambuliaji kinda Paul Peter, akifunga hat-trick yake ya kwanza tokea apandishwe.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Cioaba alisema timu hiyo itafanya bonge la ‘sapraizi’ kwa wengi kwa kupambana kuwania nafasi ya kwanza.
“Ninayo michezo mingine 15 kwenye ligi nina mipango mizuri kwenye timu kila mechi tutaenda na kucheza kwa umakini, napenda kuongea na mashabiki wetu waje kuisapoti timu, pia jana nilifurahi mashabiki wengi walikuja Morogoro niliwaona mashabiki, timu yote na wachezaji wote walifurahi,” alisema.
Alisema anakiamini kikosi chake kuwa kwa siku zijazo itapambana tena na kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi, ambao kwa sasa unashikiliwa na Simba yenye pointi 35 huku Azam FC ikiwa nazo 30.
“Mashabiki wa Azam FC wanatakiwa kujua kuwa mawazo yangu kama kocha sitarudi nyuma, nimecheza mpira huko nyuma na katika kichwa changu nimekuwa nikipenda kushinda kila wakati.
“Nimeona baadhi ya watu baada ya mechi na Yanga wamekuwa wakidhani kuwa timu ya Azam itarudi chini lakini napenda kuongea na kila mtu kuwa timu hii haitaenda chini na itapambana kwa ajili ya nafasi ya kwanza,” alisema.
Kuelekea mechi na Ndanda
Kuelekea mchezo ujao dhidi ya Ndanda utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumamosi hii saa 1.00 usiku, Kocha huyo raia wa Romania amesema kuwa kwa sasa kikosini anakabiliwa na majeruhi wawili lakini watapambana kuhakikisha wanashinda mtanange huo.
“Nina wachezaji wawili majeruhi mchezaji mwingine Sure Boy ana kadi nyekundu, wachezaji wengine waliobakia wapo tayari kwa ajili ya mechi, Daniel (Amoah) atarejea huenda akacheza sijui kwa sasa, nitamwangalia hali yake ya kimwili kesho na baada ya kesho kama atakuwa fiti kwa mchezo huo.
“Najiandaa vizuri kwa mchezo huo kiakili, kimwili na kila kitu, mazingira mazuri kwa timu na kuhakikisha tunashinda mechi na Ndanda na kuzidi kukaa juu,” alisema.
Wachezaji wengine wanaoweza kuikosa mechi hiyo kwa upande wa Azam FC ni mshambuliaji Wazir Junior, ambaye ni mgonjwa huku Joseph Kimwaga, akiendelea na programu ya mwisho ya kurejea dimbani.
Tayari kikosi hicho, kimeshaanza mazoezi rasmi leo jioni kujiandaa na mchezo huo muhimu, ambapo kimeanza mchakamchaka huo takribani saa tatu tokea kiwasili Dar es Salaam kikitokea Morogoro kilipoilaza Shupavu mabao 5-0.
Katika mchezo wa raundi ya kwanza dhidi ya Ndanda, mabingwa hao mara mbili mfululizo wa Kombe la Mapinduzi wanaodhaminiwa na Benki ya NMB, Maji safi ya Uhai Drinking Water na Tradegents, walipata ushindi wa bao 1-0 ugenini, lililofungwa na aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Yahaya Mohammed.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: