.Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo amewataka watumishi wa wizara hiyo kufanya kazi kwa bidii na  kuzingatia weledi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Dk. Akwilapo ameyasema hayo wakati wa kikao cha kwanza cha watumishi wa wizara hiyo kilichofanyika mkoani Dodoma tangu serikali itangaze rasmi kuhamishia makao makuu ya nchi mkoani humo.

Dk. Akwilapo amesema utii, ushirikiano,bidii na upendo mahali pa kazi miongoni mwa watumishi ndiyo silaha pekee ya kufikia malengo ambayo Wizara imejiwekea katika kuinua Sekta ya Elimu hapa nchini.

"Nipende kuwapongeza watumishi wote kwa kushiriki majukumu mbalimbali ya Wizara ikiwemo kuisimamia vyema miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara, nawasihi sana tuusifanye kazi kwa kujitenga, ushirikiano miongoni mwetu ni jambo la msingi sana na tukiwa na Umoja basi mafanikio lazima yatapatika katika Sekta hii ya Elimu,"alisema Dk.Akwilapo.

Pia Katibu Mkuu Dk.Akwilapo amewataka watumishi kuwa na matumizi sahihi ya Teknolojia,kujibu barua mbalimbali kwa wakati pamoja na kushughulikia faili zinazofika kwenye ofisi zao ndani siku mbili  na siyo kuziacha zikae muda mrefu.

Kupitia kikao hicho watumishi pia walipata fursa ya kuwaaga viongozi ambao walitumikia Wizara hiyo ambao hivi sasa wamehamiahiwa Wizara nyingine na kuwakaribisha viongozi wapya ambao wamehamia kwenye Wizara hiyo.

Viongozi waliokaribishwa ni pamoja na Naibu Waziri William Ole  Nasha na Naibu Katibu Mkuu Profesa  James Mdoe na walioagwa ni Naibu Waziri Mhandisi Stella Manyanya na Profesa Saimon Msanjila ambaye hivi sasa ni Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Madini.

Imetolewa na;

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

WIZARA YA ELIMU, SAYANSI  NA TEKNOLOJIA.
 17/ 2/2018.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: