Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu na chipukizi anayekua kwa kasi, Yohana Nkomola wamerejesha matumaini kwenye timu hiyo na kesho Jumamosi huenda wakawepo kwenye orodha ya kikosi kitakachoivaa St Louis ya Shelisheli.

Yanga itawakaribisha wapinzani wao hao katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Ajibu anarejea uwanjani akitokea kupona majeraha ya goti aliyoyapata kwenye Ligi Kuu Bara wakati timu hiyo ilipovaana na Azam FC na Nkomola yeye alipata maumivu ya misuli katika mchezo wa Ruvu Shooting.
 Daktari Mkuu wa Yanga, Edward Bavu, alisema wachezaji hao wameanza mazoezi magumu ya pamoja na wenzao juzi Jumatano kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar.

Bavu alisema kurejea kwa wachezaji hao kumeimarisha kikosi chao kutokana na kupunguza idadi ya wachezaji majeruhi waliokuwa wanaiandama timu hiyo.

“Niwaondoe hofu mashabiki wa Yanga kuwa, wachezaji wetu muhimu waliokuwa majeruhi Ajibu na Nkomola wamepona na jana (juzi Jumatano) walianza mazoezi ya pamoja na wenzao.

“Kwa maana hiyo hivi sasa wapo fiti kucheza mechi ya kimataifa kama kocha akihitaji kuwatumia, lakini mimi kama kocha niseme wapo fiti kwa ajili ya kuipambania timu yao ya Yanga.

“Kipa wetu Rostand (Youthe) aliyepata majeraha ya enka kwenye mechi iliyopita na Lipuli FC naye anaendelea vizuri na ameanza mazoezi ya binafsi kwa ajili ya kujiweka fiti kabla ya kuanza mazoezi magumu ya pamoja na wenzake,” alisema Bavu
Share To:

msumbanews

Post A Comment: