Hatima ya mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu Sugu anayeshtakiwa kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli itajulikana kesho.
Sugu na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga wanakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya ambayo kesho Februari 26,2018 itatoa hukumu.
Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Desemba 30,2017 eneo la Uwanja wa Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Michael Mteite anatarajiwa kutoa hukumu baada ya upande wa mashtaka na ule wa utetezi kukamilisha ushahidi Februari 9,2018.
Jamhuri iliwasilisha mashahidi watano na kielelezo kimoja cha sauti iliyodaiwa kurekodiwa na shahidi wa tano, Inspekta Joram Magova.
Upande wa utetezi uliwasilisha mashahidi sita wakiwamo Sugu na Masonga waliokana kutamka maneno wanayoshtakiwa kuyatoa.
Washtakiwa walitetewa na mawakili Sabina Yongo, Boniface Mwabukusi na Hekima Mwasipu kabla ya kujitoa na sasa wanawakilishwa na Peter Kibatala.
Kwa mara ya kwanza, Sugu na Masonga walifikishwa mahakamani Januari 16 na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph Pande aliyeeleza upelelezi ulikuwa umekamilika na walikuwa tayari kuendelea na usikilizaji
Post A Comment: