Kampeni za ubunge jimbo la Kinondoni zimeingia siku ya 12 leo Februari Mosi, 2018 huku mgombea wa TLP, Dk Godfrey Malisa akijinadi kwa kubainisha akiwa mbunge hawezi kuhamia chama kingine cha siasa na kusababisha uchaguzi Kinondoni kurudiwa.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la stendi ya zamani Mwenge, Dk Malisa amesema hawezi kufanya kitendo alichokifanya mgombea wa CCM, Maulid Mtulia aliyejivua uanachama CUF na kupoteza ubunge wa Kinondoni. Mtulia alihamia CCM Desemba 2017 ambako alipitishwa tena kuwania ubunge wa jimbo hilo.
“Uchaguzi huu na hasara itakayotokea ni kwa sababu ya mtu mmoja Mtulia. Msimchague mtu wa aina hiyo. Siwezi kuwadhalilisha wana Kinondoni kama alivyowafanyia Mtulia. Mwaka 2015 Ukawa walisimama pamoja kumnadi  Mtulia sasa hivi Ukawa wamesambaratika kina mmoja anamnadi mgombea wa chama chake, kumetokea nini,” amesema Dk Malisa.

Ameongeza, “Naomba kura zenu kama mnataka jimbo hili liendeleee kubaki kwa wapinzani. Hao wenye undugu na Ukawa msiwape kura watawatosa kama alivyofanya Mtulia. CCM, Chadema  na CUF  msichague vyama chagueni mtu mwenye uwezo na msomi ambaye ni Malisa
Wakati Dk Malisa akitumia gia ya kuhama Mtulia kujinadi, Mtulia amefanya mkutano katika viwanja vya Msisiri na  amezungumzia mambo mbalimbali ya maendeleo na kuwajibu wanaomshangaa kuhamia CCM.

Amesema wapo watu wanamuona mjinga kuacha kiinua mgongo bungeni.

 “Nimejitoa kafara kwa ajili ya kutetea maslahi yenu ambayo kuyatekeleza kule nilikokuwa isingekuwa rahisi. Wanaoniita mie msaliti kwa sababu nimekuja CCM, nimekuja kwa sababu ya wananchi wangu,” amesema Mtulia na kuongeza,

“Mbona hawajaungana pamoja kunishambulia  mimi msaliti badala yake wamesambaratika na kuturahisishia kazi CCM. Nilidhani wao wasiokuwa wasaliti wangefanya kitu tofauti, matokeo yake wamesambaratika na kulumbana wao mwa wao.”

Mtulia amesema CCM itatoa fedha fedha ya kujenga barabara zenye mashimo na mpaka mwisho wa mwezi huu, wanawake na vijana watapata Sh30milioni.

Kabla ya kumnadi Dk Malisa, Mwenyekiti wa TLP, Agustino Mrema amesema, “Mliosema nimekwisha wakati rais ananipa madaraka ni kama mmechanganyikiwa akili.”

“Lengo la Rais Magufuli sio kuua vyama. Vyama vyenyewe ndiyo vina wanachama wababaishaji. Rais ni rafiki yangu kanipenda nikiwa TLP yeye akiwa CCM huyu ndiye rafiki wa kweli. Watu wanahamia CCM kwa sababu ya umahiri wa rais Magufuli siyo kwamba anawahonga.”

Amesema Ukawa wanamnyanyapaa na kumuita mzee,  kubainisha kuwa vyama vinavyounda umoja huo havitapata kura za wazee wa Kinondoni.

 “Wananishangaa kwanini nampenda Rais,  ni mjinga pekee ndio anaweza asimpende Magufuli.  Wapinzani wenzangu hawanipendi  mimi nitawapenda vipi? Ndio maana namuunga mkono rais,” amesema.

Mgombea wa CUF katika jimbo hilo, Rajab Salim Juma amesema, “Wagombea wengine siyo wenyeji wa jimbo hili, hawajui shida za wananchi. Mwingine alipewa dhamana lakini ameshindwa kuitumikia. Naomba kura zenu niwalipe maendeleo.”

Naye Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Abdul Kambaya wakati akimnadi Juma amesema, “Tumegawanywa na mfumo ndiyo maana hata walio polisi ni watoto wa masikini. Huwezi kukuta mtoto wa kigogo akiwa polisi, wao wako BOT (Benki Kuu ya Tanzania). Wakazi wa Kinondoni tuungane kuuvunja huu mfumo.”

Akiwa katika kata ya Ndugumbi, Manzese mgombea wa Chadema, Salum Mwalimu ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), amesema katika kata ya Ndugumbi eneo la Mikoroshini, linakumbwa na mafuriko ya mara kwa mara, kuahidi kuibomoa moja ya nyumba iliyojengwa katika njia ya maji.

“Nawahidi nikichagulia nitatoa Sh1Omilioni kwa mmiliki wa nyumba hiyo ili michakato ya kuivunja uanze sanjari kumtafutia kiwanja sehemu atakayoipenda,” amesema.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: