Wakili Fatma Karume na Mtoto wa aliyekuwa Mbunge Tarime, Chacha Wangwe, Bob Wangwe wamefunguka na kusema kuwa wamepanga kufungua kesi kupinga Wakurugenzi kusimamia uchaguzi nchini.
Akiongea na waandishi wa habari Fatma Karume amesema kuwa Tanzania sasa baadhi ya viongozi waliwahi kusikika wakijinadi kushinda uchaguzi hata kwa magoli ya mkono na kudai kuwa haki ya kura sasa inaonekana kama haina thamani, hivyo wao wanataka kuipigania haki hiyo kupitia sheria ili ipatikane.
Aidha Fatma Karume amesema watu ambao waliweka mfumo huo wa Wakurugenzi kuwa wasimamizi wa uchaguzi walikuwa na lengo lao na walifanya hivyo kwa kuwa walikuwa wanajua nini wanataka kufanya.
"Mtu akipiga kura haina thamani yoyote na matakwa yake hayasikilizwi kwa sababu kuna kitu kinaitwa goli la mkono, sasa kama kuna goli la mkono linatoka kwenye mfumo, kama kwenye mfumo kuna refa anaona, refa wa haki hawezi kukubali goli la mkono lakini tukajiuliza ni nini kinafanya refa afunge macho au asione watu ambao wanasema wao watashinda kwa goli la mkono. Kila mtu ana haki ya kupiga kura na kura yake ihesabike sasa kama kuna watu wanapiga magoli ya mkono haki yako hii inachukuliwa yaani imetekwa"
"Chini ya Katiba yetu refalii wa masuala haya ni Tume ya Uchaguzi, Katiba inasema huyo refalii lazima awe mtu ambaye hayumo kwenye chama chochote cha kisiasa siyo CHADEMA, CCM wala CUF bali anatakiwa awe mtu ambaye si mwanachama wa chama chochote, kwa hiyo msimamizi wa uchaguzi ni marufuku kuwa chini ya chama chochote kwa mujibu wa Katiba yetu yaani kuna matatizo makubwa ya sheria hapa lakini mwisho unakuta unakuta kwamba wasimamizi wa kura wanavaa magwanda ya chama siku moja siku ya pili wanavaa sare za sare za Tume ya Uchaguzi halafu wananchi wanalalamika, na wananchi wanalalamika kwa sababu ya mfumo na mfumo umewekwa kisheria na watu walioweka huo mfumo wanajua wamefanya nini" alisema Fatma Karume
Kufuatia mapungufu hayo ya Sheria Fatma Karume amesema kuwa alichokigundua yeye magoli ya mkono yanatokea kwa sababu ya mfumo na kwa mfumo huo hizo kura zitapigwa kila siku hivyo ameshauri waende mahakamani kuhoji mahakama kama mfumo huo unakubalika chini ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inataka kila kura ihesabike, na katiba inayotaka Demokrasia.
Post A Comment: