“Niseme tu mambo yameenda vizuri na kama mnavyojua mambo ya mahakamani ikitokea ninahitajika nitakuja,” amesema.
Diamond alifika mahakamani hapo leo Februari 8, 2018 kusikiliza kesi inayomkabili ya matunzo ya mtoto Prince Abdul iliyofunguliwa na Mobeto.
Amesema yeye na Mobeto hawana shida yoyote, ila kuna watu waliokuwa wakizungumza maneno na kumchochea Mobeto.
"Tunahitaji kuweka mambo sawa. Tunahitaji kuwa katika mstari kwa sababu vitu vidogo vinaharibu upande wa mama na upande wa baba kwa hiyo tulikuwa tunaweka mambo sawa ili kesho na keshokutwa yasilete sintofahamu baina yetu,” amesema na Diamonda na kuongeza:
“Ikitokea kuna mtafaruku baina ya mtoto, kila mtu anakuwa na mawazo yake, kwa hiyo ni lazima kumjenga mtoto na kuhakikisha kuwa mtoto anajengwa na kulelewa katika malezi bora.”
Alipoulizwa ni kiasi gani cha fedha anachoweza kumudu kutoa kwa ajili ya matunzo ya mtoto huyo, amesema kiasi cha fedha kinazungumzwa zaidi lakini mtoto anahitaji matunzo mengi.
"Kiasi cha pesa tunachoandika sehemu kama hizi tunazungumza tu. Mtoto ana mahitaji mengi wakati mwingine mtoto wako unaweza kumpa hata Sh100 milioni. Huwezi kusema siwezi kumpa kwa sababu niliandikisha nitampa Sh100,000. Tumeweka mazingira mazuri ya kiasi kitakachomfanya akue katika malezi bora,” amesema.
Msanii huyo amesema kupitia kesi hiyo amejifunza vitu vingi na kwamba, mazungumzo yao ndani ya mahakama hiyo ni siri yao: “mambo yamekwisha.”
Amesema atahakikisha mtoto huyo anakuwa katika mazingira mazuri, kumsomesha kadri ya uwezo wake utakavyoruhusu kwa maelezo kuwa maisha ni kupanda na kushuka.
“Kuna wakati unakuwa hauna unasema leo mie sina basi mambo yanakuwa Bundasiliga leo mnakula mihogo maisha ndivyo yalivyo,” amesema.
Post A Comment: