Katibu Tawala Wilaya ya Arumeru  Timoth Mzava amelazimika  kutoa maelezo ya kina juu ya tamko la mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli juu ya uchangiaji wa chakula kwa wanafunzi wa shule za kutwa wakati wa Mkutano wa Baraza la Madiwani wa kuwasilisha taarifa za kata kwa robo ya pili mwaka wa fedha 2017/2018.

Mkutano huo uliotawaliwa na mjadala mrefu wa ulioibuliwa na baadhi ya wajumbe juu ya uchangiaji wa chakula cha mchana kwa wanafunzi wa shule za kutwa , uchsngiaji uliyozua  ya sintofahamu kwa wazazi baada ya tamko la hivi karibuni la  mheshimiwa rais wa Dkt. John Magufuli.

Katibu Tawala huyo amefafanua kuwa agizo la Mheshimiwa Rais liko wazi na halijafuta wala kutengua  waraka namba 5 na 6 wa mwaka 2015 wa Elimu bila malipo ulioainisha majukumu ya serikali, halmashauri, shule, wazazi na jamii kwa ujumla katika ushiriki wa elimu.

               Awali  Diwani wa Kata ya Matevesi Mheshimiwa Julius Mollel aliomba kupata maelezo na ufafanuzi juu ya upatikanaji wa chakula cha mchana kwa wanafunzi wa shule za kutwa kufuatia tamko la mheshimiwa Rais ambao umepokewa kwa mitazamo tofauti na wananchi wengi kiasi cha  kuathiri utaratibu uliokuwepo wa uchangiaji na kusababisha baadhi ya wazazi kudai fedha zao walizokwishachangia.

         Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya Arusha Mheshimiwa Baraka Simon alimtaka Katibu Tawala wilaya ya Arumeru kutoa ufafanuzi wa suala hilo  la uchangiaji wa chakula cha wanafunzi wa kutwa kwa kuzingatia changamoto walizotoa wajumbe.

       Naye Katibu Tawala Mzava ameeleza kuwa agizo la Mheshimiwa Rais liko wazi na halijafuta waraka namba 5 na 6 wa mwaka 2015 wa Elimu bila malipo ulioainisha majukumu ya serikali katika kuchangia elimu, majukumubya halmashauri, majukumu ya Kamati na Bodi za shule pamoja na majukumu ya  wazazi na jamii.

       Waraka huo umeainisha moja ya jukumu la mzazi na jamii ni kuhakikisha wanafunzi wa shule za kutwa wanapata chakula cha mchana wawapo shuleni kwa makubaliano yao wenyewe ya namna sahihi ya upatikanaji wa chakula hicho.

        Aidha Katibu Tawala huyo ameweka wazi kuwa Mheshimiwa Rais hajazuia michango hiyo bali amesisitiza aina yoyote ya makubaliano ya michango isiathiri uwepo wa mwanafunzi shuleni na walimu wasihusike na aina yoyote ya uchangishaji na utunzaji wa  michango hiyo.

        "Wazazi na jamii wa eneo husika watakapoona inafaa wanaruhusiwa kukaa na kukubaliana namna nzuri ya kuchangishana muwasilishe Mkurugenzi lakini isije ikawa ni utitiri wa michango ili watoto wao wapate chakula wawapo shuleni lakini walimu hawaruhusiwi kujihusisha kwenye michango hiyo na zaidi hairuhusiwi mwanafunzi kubughudhiwa kwa namna yoyote ile awapo shuleni" amefafanua Mzava

        Hata hivyo  Katibu Tawala huyo ametolea ufafanuzi juu ya kuzuia kwa muda kuchangisha michango ya maendeleo kwenye kata na vijiji ili kuweka utaratibu mzuri wa usimamizi  wa fedha zinazochangwa na wananchi na kupata taarifa sahihi za mapato na matumizi ya fedha hizo.

       "Tumezuia uchangishaji wa fedha kwenye kata na vijiji ili kuweka sawa taratibu za usimamizi wa fedha zinazochangishwa baada ya kugundua ubadhilifu katika matumizi ya fedha hizo kwenye baadhi ya maeneo" amesema Mzava 

      Amewathibitishia madiwani hao kuwa kibali hicho kitatolewa mapema kabla ya mwisho wa mwezi huu na kuwapa nafasi wananchi kuendelea kushiriki uchangiaji wa shughuli za maendeleo katika maeneo yao na kuwa na miongozo yenye kuwahakikishia matumizi halali ya fedha zao. 

Pia Mzava amewataka Madiwani hao kuacha kutumia lugha za kuudhi na kuikashifu serikali kwani inafanya kazi kubwa sana kuwaletea watu wake maendeleo.

Awali Wajumbe wa Baraza la Madiwani halmashauri ya Arusha wamefanya Mkutano wa kuwasilisha taarifa za kata za robo ya pili za kuanzia mwezi Oktoba mpaka Disemba 2017 mkutano uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa halmashauri hiyo.

    Aidha  Madiwani wa kata zote 27 wamepata fursa ya kuwasilisha taarifa za kata zao huku taarifa hizo zikionyesha shughuli za maendeleo katika kata, hali ya chakula, Elimu,Afya, Maji, Miundombinu ya barabara, pamoja na taarifa za ulinzi na usalama.
Share To:

Post A Comment: