SIRI imefichuka, kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinashirikiana na baadhi ya viongozi serikalini, kumtumia msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Sales Katabazi Mutungi, ili kuvifuta vyama viwili vikubwa vya upinzani nchini.

Taarifa zinasema, vyama ambavyo viko kwenye mkakati wa kuvifuta, ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF).

Vyama vya Chadema na CUF, kwa sasa ndivyo vyama vikuu vya upinzani nchini.

Wakati CUF ikitikisa Zanzibar, Chadema kimeshika usukani Tanzania Bara; na ni miongoni mwa vyama vinne vinavyounda jumuiko la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

“Ndio kuna mkakati wa kutaka kuvifuta vyama viwili vikubwa vya upinzani nchini. Mkakati huu, unaratibiwa na baadhi ya viongozi wa CCM, wanaoshirikiana na wale wa serikali,” ameeleza mfanyakazi mmoja wa ofisi ya msajili kwa sharti la kutotajwa gazetini.

Amesema, “lengo la mpango huu, ni kwamba hadi kufikia mwaka 2020, tunapokwenda kwenye uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, hakuna chama kikubwa cha upinzani nchini.”

Kupatikana kwa taarifa hizi kumekuja wiki moja baada ya msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi, kuitaka Chadema kujieleza ndani ya siku tano, kwa nini kisifutwe kwenye daftari la usajili wa vyama siasa nchini.

Jaji Mutungi ameituhumu Chadema kuwa imekiuka kifungu cha 9(2) cha sheria ya vyama vya siasa na kanuni ya 6(1)(b) ya maadili ya vyama hivyo.

Katika barua yake kwa katibu mkuu wa Chadema, Jaji Mutungi anadai kuwa chama hicho kilifanya maandamano, tarehe 16 Februari 2018 na kusababisha vurugu na baadaye kifo cha Akwilina Akwiline.

Akwilina alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika chuo cha usafirishaji cha taifa (NIT). Alipigwa risasi inayodaiwa kurushwa na askari wa jeshi la polisi akiwa ndani ya daladala, tarehe 16 Februari.

Aidha, kupatikana kwa taarifa hizi kumekuja wiki moja baada ya jeshi la polisi Visiwani, kuvamia makao makuu ya CUF yaliyopo Mtendeni, Unguja kwa lengo la kufanya upekuzi.

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, ameita upekuzi huo, kuwa “ni dhamira ovu sana kwa chama” chake.

Upekuzi kwenye makao makuu ya CUF ulifanyika tarehe 20 Februari 2018. Ulianza saa 12:20 jioni hadi saa 1:30 usiku.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir Ali, amekiri kufanyika kwa upekuzi huo.

Alisema, jeshi lake limelazimika kuzipekua ofisi za chama hicho, baada ya kupokea taarifa kuwa “ndani ya ofisi hizo kumehifadhiwa silaha, jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya vyama vya siasa.”

Alisema, “…baada ya kufanya ukaguzi na kubaini hakuna kitu, tulisaini kuwa tumefanya ukaguzi na hatujagundua kitu chochote cha hatari kinyume cha tulivyopata taarifa. Askari wote waliokuwa wakifanya ulinzi katika eneo hilo tuliwaondoa.”

John Mnyika, naibu katibu mkuu wa Chadema ameliambia gazeti hili kuwa chama chake kimepata taarifa hizo, lakini akaonya kuwa “mkakati huo, hauwezi kufanikiwa.”

Anasema, “tunaelewa. Msajili anasukumwa na serikali kufanikisha dhamira yao ni kukifuta Chadema. Nawaambia hivi, jambo hilo hawaliwezi.”

Juhudi za kumpata Jaji Mutungi kuzungumzia madaia hayo, hazikuweza kufanikiwa. Mara mbili, mwandishi alipiga simu yake, lakini haikuweza kupokelewa.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, mpango wa kuvifuta vyama hivi, utaanzia Chadema na baadaye kufutwa kwa CUF; vyama hivyo vitafutwa kabla ya kumalizika kwa mwaka huu.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: