WIMBO wa 'Subalkheri Mpenzi', ulioimbwa na wasanii wa kizazi kipya Aslay Ishack na Nandy, umezidi kuzua utata  baada ya mmiliki wa wimbo huo, Kikundi cha Tarab Asilia visiwani Zanzibar (Culture Music  Club), .........

Kudai kuwa watawaburuza mahakamani kwa kuwa Sh. 800,000 zilizotolewa kama fidia hawazitambui.

 Akizungumza na Nipashe jana, Katibu Mtendaji wa kikundi hicho, Taimur Rukuni Twaha, alisema wasanii hao kabla ya kuimba tena upya wimbo huo walipaswa kuonana na uongozi huo ili kukubaliana jambo ambalo hawakufanya hivyo.

Kwa mujibu wa katibu huyo, wasanii wa kikundi hicho waliopewa mgawo huo wa fedha ni waimbaji wawili (majina tunayo) ambao mmoja alipewa Sh. 500,000 na mwingine Sh. 300,000.

“Walichokifanya Aslay na Nandy kwenda kwa waimbaji wetu na kuwapa kiwango hicho cha fedha kwetu tunaona hakikubaliki na wametoa kama zawadi tu kwa sababu thamani ya wimbo wetu haulingani na kiwango hicho,” alisema Twaha.

Alisema kwa mujibu wa katiba ya kikundi hicho, ibara ya sita inaeleza nyimbo zote zilizoimbwa na kikundi ni mali ya kikundi na kwamba  muimbaji, mtunzi na muweka sauti watakuwa na haki zao kupitia kikundi hicho.

Alisema kimsingi msimamo wao utabaki pale pale wa kuwafikisha mahakamani wasanii hao endapo watashindwa kutimiza masharti waliopewa na uongozi wa kikundi hicho.

Aidha, alisema masharti hayo hayatomhusu Aslay na Nandy peke yao bali na mwanamuziki Hussein Mmanga Faki (maarufu HamaQ) na mwenzake Mosi Suleiman kwa kuimba wimbo wa 'Mke wa Awali ni Wewe Aziza' ambao pia ni mali ya kikundi hicho.

“Tunafahamu kuwa nyimbo zetu wameziimba tena kwa lengo la kibiashara na wamekuwa wakipata fedha kupitia nyimbo hizo,”alisisitiza katibu huyo.

Alisema tayari wameshawaandaa mawakili wao, ambao wataisimamia kesi hiyo mahakamani iwapo wasanii hao watashindwa kutimiza masharti waliyopewa.

Akizungumzia suala hilo, Meneja wa Coconut FM, ambaye ni mwakilishi wa Aslay na Nandy, alisema kuwa wasanii hao watafikishwa katika uongozi wa Kikundi cha Taarab Asilia (Culture) ili kupata suluhu.

Alisema wao hawana makosa kutumia wimbo huo, kwani kabla ya kurudia kuuimba walishakutana na mtunzi wa wimbo huo Bakari Abeid ambaye sasa ni marehemu na kumalizana naye wakati wa uhai wake.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: