Kesi ya mfanyabiashara wa mkoani Morogoro, Focus Munishi anayeshtakiwa kwa kumjeruhi kwa kumtoboa jicho mwanamke aliyekuwa mpenzi wake, Nanjiva Geofrey imeanza kusikilizwa Mahakama Kuu.
Katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Rehema Sameji, upande wa mashtaka unaongozwa na wakili wa Serikali, Sunday Hyera huku wa utetezi ukiongozwa na Benjamin Jonath.
Awali, akisoma maelezo ya shtaka, Hyera alieleza kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Septemba 15, 2016.
Wakili Hyera alidai kuwa bila uhalali huku akijua kufanya hivyo ni kosa, mshtakiwa huyo alimpiga Nanjiva kisha kumtoboa jicho kwa kutumia kiatu chake kirefu (highhills) na hivyo kumsababishia madhara yaliyosababisha jicho hilo kupata ulemavu wa kudumu.
Alidai kuwa upande wa mashtaka tayari umekamilisha upelelezi na unategemea kuwa na mashahidi tisa pamoja na vielelezo saba.
Kesi hiyo imehairishwa hadi itakapopangwa tena kwenye kikao kingine cha Mahakama Kuu huku mshtakiwa akiwa nje kwa dhamana.
Post A Comment: