Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo),  Zitto Kabwe amesema amepatikana mwekezaji wa kujenga maduka makubwa la biashara (malls) mkoani humo kama yale ya  Mlimani City ya jijini Dar es Salaam.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Community Center, Mwanga leo Januari 20, 2018,  Zitto amesema haiwezekani mkoa wa Kigoma ukaendelea kubaki nyuma kimaendeleo.
Zitto ambaye pia ni Kiongozi wa ACT- Wazalendo amesema inapofika jioni mji wa Kigoma unakuwa kimya jambo alilodai kuwa haliwezi kuleta mabadiliko na kukuza mzunguko wa fedha.

 “Tumepata mwekezaji wa kujenga mall kubwa kama ya Mlimani City ili ikifika usiku kuwe kumechangamka. Hatuwezi kuendelea kuwa mkoa au mji wa mwisho,”  amesema Zitto na kuongeza,

“Haina maana sisi watoto wenu kusomeshwa na kuuacha mji huu ukaendelea kuwa hivi. Tunahangaika, mtuache tufanye kazi na mwaka 2020 mtaniuliza kupitia kile nilichoahidi na mtaninyonga kwa nilichowaahidi.”

Kuhusu mapato ya halmashauri ya Kigoma Ujiji, Zitto amesema kitendo cha Serikali kuu kuchukua vyanzo vya mapato vilivyokuwa vikiiingizia mapato halmashauri hiyo na kutekeleza mipango yake,  imewalazimu kuongeza kodi kwa wafanyabishara.

“Tukiwaumiza kidogo katika kodi tuvumiliane na mimi sitawaangusha lakini huwezi kwenda peponi bila kufa, kwa hiyo lazima tuumie kidogo na nitakuwa kiongozi mwongo nikija hapa na kusema kila kitu mtapata ni uongo,” amesema Zitto na kuongeza,
“Sisi hatuna wa kutubeba. Lazima tupambane wenyewe na tutiane moyo. Hakuna jambo baya tunapopambana kuleta maendeleo lakini wengine wanaturudisha nyuma, haipendezi, tutiane moyo jamani.”
Amesema lengo ni kuubadili mji wa Kigoma kwa kuwa umekuwa nyuma kwa muda mrefu.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: