WAKATI mshambuliaji wa kimataifa wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, Obrey Chirwa akirejea uwanjani kuivaa Azam FC katika mchezo utakaopigwa keshokutwa, timu hiyo itamkosa straika wake anayekuja juu, Pius Buswita.

Chirwa anarejea tena uwanjani baada ya kumaliza kutumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu aliyopewa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutokana na kosa la kumpiga mchezaji wa Prisons wakati timu hizo mbili zilipokutana kwenye mchezo wa raundi ya kwanza Novemba mwaka jana.

Akizungumza Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema Buswita, ataukosa mchezo huo kutokana na kupaswa kuwa nje kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano ambazo ameonyeshwa.
Saleh alisema kuwa kikosi chao kinafuraha kuona beki wake wa kati mkongwe, Kelvin Yondani, ambaye alikuwa anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano akirejea uwanjani. Beki huyo alikaa nje wakati Yanga ikicheza na Ruvu Shooting Jumapili.

"Maandalizi yetu yanaendelea vizuri, lakini Jumamosi tutamkosa Buswita, ila Chirwa na Yondani wamemaliza adhabu," alisema kwa kifupi meneja huyo.
Baada ya mechi hiyo ya Jumamosi, Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, itakuwa imemaliza mzunguko wa kwanza wa ligi na itajiandaa kuwafuata Lipuli katika mchezo wa raundi ya 16 utakaopigwa Februari 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Samora mkoani Iringa.

Simba ambayo nayo inadhaminiwa na SportPesa, ndiyo vinara katika msimamo wa ligi wakiwa na pointi 32 wakifuatiwa na Azam FC yenye pointi 30 wakati mabingwa watetezi Yanga wako katika nafasi ya tatu baada ya kufikisha pointi 25 sawa na Mtibwa Sugar na Singida United inakamilisha Tano Bora ikiwa na pointi zake 24.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: