Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce  Ndalichako amesema Serikali haijakataza uchangiaji wa hiari na kuwa kilichokatazwa ni michango ya lazima ambayo imekuwa kero kwa wazazi kwani imekuwa kama kiingilio, ambapo mtoto haruhusiwi kuingia shuleni kabla mzazi hajalipa michango hiyo.


Waziri Ndalichako amesema Serikali haizuii wananchi kwa hiari yao wenyewe kuchangia Maendeleo ya Elimu ya watoto wao iwapo michango itakusanywa kwa utaratibu uliowekwa  na kuratibiwa na mmoja wa wazazi na siyo mkuu wa shule.


Waziri Ndalichako ametoa kaui hiyo  mjini Makambako mkoani Njombe wakati akishiriki  uzinduzi wa kampeni ya upimaji wa kansa ya matiti na mlango wa kizazi, kifua kikuu na magonjwa mengine yasiyoambukiza kampeni ambayo iliratibiwa na mkoa huo wa Njombe.


Akikagua ujenzi wa mabweni unaoendelea katika shule ya sekondari Sovi iliyopo mkoani Njombe Waziri Ndalichako amekiri kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa mabweni hayo ambapo aliwasifu wananchi  kwa kazi nzuri inayofanywa na viongozi wao wa mkoa.


Waziri Ndalichako amewataka  wananchi kuendelea na moyo wa kuchangia Ujenzi huo na kamwe wasikatishwe tamaa na uvumi uliopo kuwa hawaruhusiwi kuchangia maendeleo yao ya Elimu ya watoto wao.


Akiwa Wilayani Makete Waziri Ndalichako aliamrisha kusimamishwa Ujenzi  wa chuo cha ufundi  stadi VETA kwa kuwa  gharama zilizotajwa zipo juu sana na hazina uhalisia, ambapo amemuagiza Meneja wa VETA wa kanda kwa kushirikiana na mhandisi wa Halmashauri asimamie ili gharama hizo ziangaliwe upya.

Waziri Ndalichako alisikitishwa  kuona ujenzi haujaanza mpaka sasa japo kuwa mkataba wa kazi hiyo ulisainiwa  Agosti, 2017 na kazi ya Ujenzi kukabidhiwa kwa Mkandarasi ambaye ni  Wakala Wa Majengo - TBA   Oktoba 2017.


Pia Waziri Ndalichako amemuagiza Katibu Mkuu  wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dk. Leonrd Akwilapo kutuma  Mkaguzi ili afuatile matumizi ya fedha ya mradi huo.


Imetolewa na;

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

26/1/2018
Share To:

msumbanews

Post A Comment: