WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Bibi Anna Mghwira asitishe uuzwaji wa mali za Chama cha Ushirika cha Kilimanjaro (KNCU).
Ametoa agizo hilo jana jioni (Jumatano, Januari 17, 2018) wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Serengeti, wilayani Tarime.
Hatua hiyo imekuja baada ya KNCU kutangaza kuuza shamba lake kwa ajili ya kuiwezesha benki yake ya KCBL kutimiza sharti la mtaji la Benku Kuu ya Tanzania (BoT).
Benki hiyo ya KCBL inatakiwa kutimiza sharti la kuwa na mtaji kamili unaotosha wa shilingi bilioni tano (5) katika kipindi cha miezi sita tangu kutolewa kwa tangazo hilo.
Waziri Mkuu alisema ni marufuku kuuza mali za Ushirika huo, hususan katika kipindi hiki ambacho Serikali inafanya uhakiki wa mali za vyama mbalimbali vya Ushirika nchini.
Alisema Serikali imedhamiria kuimarisha Ushirika nchini na sasa inafanya uhakiki wa mali za vyama vya Ushirika na watakaobainika kuhusika na ubadhilifu watachukuliwa hatua.
Januari 4, 2018 BoT ilizipa miezi sita benki tatu ili ziweze kuongeza kiwango cha mtaji unaohitajika kutokana na matakwa ya kisheria ya kuwa na mtaji kamili wa kutosha.
Benki hizo ni Kilimanjaro Co-Operative Bank Limited, Tanzania Women Banki Plc na Tandahimba Community Bank Limited, zitakaposhindwa kutekeleza agizo zitachukuliwa hatua.
BoT ni itazifutia leseni na kusimamisha shughuli za kibenki chini ya ufilisi, iwapo benki hizo zitashindwa kutekeleza agizo hilo ihadi kufikia Juni 30, 2018.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Post A Comment: