Jaffo aliyasema hayo jana katika viwanja vya Sanya Juu wakati akimnadi mgombea ubunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Godwin Mollel, ambaye hivi karibuni alijiondoa Chadema na kugombea tena nafasi hiyo kupitia chama tawala.
Jaffo alisema chama hicho ndicho chenye Serikali na ndicho kinachoweza kutatua changamoto na shida za wananchi.
Alisema endapo Dk Mollel atashinda, Serikali itafanya kila liwezekanalo ili kuhakikisha Siha inasonga mbele kimaendeleo na maisha ya wananchi yanaboreshwa.
Jaffo aliwataka wananchi wa jimbo hilo kumchagua Dk Mollel ili kuisukuma Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi.
“Mollel ni kiongozi makini, mpeni ridhaa ili Serikali tushirikiane naye kuwaletea maendeleo na ninawahakikishia mkimchagua, miaka miwili iliyobaki Siha itakuwa moja ya wilaya ambazo zitapiga hatua kubwa na kufanya vizuri katika utekelezaji wa maendeleo,” alisema.
“Naomba msifanye makosa maana tutashughulika na shida na changamoto zote za wananchi, tutatatuta tatizo la maji, tutaboresha huduma za afya, elimu, barabara na kuwafanya wananchi kupata huduma zote muhimu za kijamii.”
Akimnadi Dk Mollel, katibu wa itikati na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole mbali na kuwaomba wananchi wa Siha kumchagua Mollel aliwataka wanasiasa kuacha kutumia shida za wananchi kama mtaji wa kisiasa.
“Muda wa kufanya siasa za uwongo umepitwa na wakati, sasa tufanye siasa za kushughulika na shida za wananchi, tuboreshe maisha na kusogeza karibu na wananchi huduma za kijamii na tusigeuze maisha ya watu kuwa mtaji wa kisiasa,” alisema Polepole.
Alisema maendeleo hayana vyama, hivyo kuwataka wananchi kumchagua Dk Mollel, ambaye amehamia timu ya ushindi ambayo ina uhakika wa kuwaletea maendeleo.
Akiomba kura, Dk Mollel alisema alivua gwanda ili aweze kushughulika na shida za wananchi na hivyo akawaomba wananchi kumpa kura zote za ndio.
Aliwaambia wananchi kuwa anatambua mchango wao wa mwaka 2015, hivyo wamrudishe ulingoni ili akatatue changamoto zinazowakabili, ambazo alishindwa kuzitatua akiwa upinzani.
“Natambua mchango wenu katika ubunge nilioupata 2015, lakini mlinituma kusoma ramani ya maendeleo na niliona nilikokuwa kulinituma katika ramani ya vijiweni na ndio maana nimeingia huku ambapo naona ramani ya maendeleo inasomeka vyema, hivyo nipeni kura zote ili nikatekeleze,” alisema.
Alisema akichaguliwa Februari 17,atashirikiana na Serikali kuhakikisha wanatatua changamoto zinazowakabili, ikiwemo tatizo la maji, miundombinu ya shule, barabara na migogoro ya ardhi.
Post A Comment: