Hofu ya watu wasiojulikana imezidi kutanda katika jamii mara baada ya kutekwa kwa vijana 10 ambao ni madereva boda-boda katika eneo la Njiapanda ya Neruka, Mtoni Kijichi Jijini Dar es salaam, kushikiliwa na kupigwa kwa saa sita kisha kuachiwa.
Tukio hilo linadaiwa kutokea juzi saa tatu asubuhi baada ya watu watano wenye silaha kufika katika eneo hilo na kuwachukua vijana hao na kuwapeleka kusikojulikana kisha kuwaachia saa kumi jioni.
Akizungumza kwa niaba ya vijana wenzake waliotekwa mmoja wa vijana hao na kucharazwa viboko, Augustino Januari amesema kuwa juzi saa tatu asubuhi walifika watu watano wakiwa katika gari aina ya Prado Tx lenye rangi ya bluu na kuwaamuru wapande ndani ya gari hilo.
“Tulipakiwa pale watu 10 na wao walikuwa watano kila mmoja akiwa na bastola na ndani ya gari kulikuwa na silaha nyingine kubwa SMG, tuliamliwa kuvua mashati na wakatufunga usoni na kutupeleka kwenye nyumba ambayo hatukuifahamu, ndipo walipoanza kutucharaza bakora,”amesema Januari
Hata hivyo, Augustino amesema kuwa watu hao walikuwa wakihitaji kiasi cha shilingi milioni 2 ambazo wanadai kuwa waliibiwa Kompyuta Mpakato (Laptop) na nyaraka muhimu katika Bar moja kubwa eneo hilo, kitu ambacho amesema waliomba msaada kwa ndugu zao na kufanikiwa kupata kiasi hicho cha fedha kisha kuachiwa.
Post A Comment: