Watuhumiwa 24 kati ya 61 wanaokabiliwa na kesi za ugaidi jijini hapa wamehukumiwa kifungo cha miezi sita jela kwa kosa la kuvua nguo na kisha kugoma kuingia ndani ya chumba cha mahakama kusikiliza kesi zinazowakabili.
Hukumu hiyo imetolewa leo Januari 30 katika mahakama ya hakimu mkazi Arusha na hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Nestory Baro ambapo amesema kwamba watu hao wamehukumiwa kwa mujibu wa kifungu nambari 114 (a) cha mwongozo wa mashtaka ya jinai.
Hata hivyo, baada ya hukumu hiyo baadhi ya watuhumiwa wamevua nguo zao na kubakisha nguo zao za ndani wakati wakipandishwa kwenye karandinga wakati wakirejeshwa katika gereza kuu la mkoa wa Arusha.
Awali kabla ya kusoma hukumu hiyo mwendesha mashtaka wa Serikali ,Augustino Kombe ameiomba mahakama hiyo iwachukulie hatua kali na kutoa adhabu kwa watuhumiwa wa kesi hizo wanaogoma mahakamani.
Mara baada ya kauli hiyo ndipo Hakimu Baro akasema kwamba anatoa kifungo cha miezi sita kwa watuhumiwa hao ili iwe fundisho kwa wengine watakaoonyesha vitendo hivyo ambavyo amesema sio vya kistaarabu.
“Kugoma sio ustaarabu kabisa halafu tuone mwisho wake hili ni fundisho kwa wote watakaogoma tena sasa muende jela miezi sita halafu mrudi na zile nguo za magereza” amesema Baro
Waliohukumiwa ni Rajabu Yakubu, Swalehe Hassan, Anwar Mashali, Jafari Lema, Abdul Hamid, Mgaya Mgaya, Abdallah Rabia, Hassan Said, Abdallah Juma, Maka Gewa, Sudi Nassib na Swalehe Hamis.
Wengine ni pamoja na Hamad Issa,Yassin Mohammed, Hamad Yahya, Juma Nguli, Khalid Makame, Shaban Wawa, Yassin Sanga, Ally Hamis, Ibrahim Lend, Rajab Hemed, Shaban Masu sanjari na Mohammed Nuru.
Mara baada ya kutoa hukumu hiyo Hakimu Baro aliahirisha kesi inayowakabili watuhumiwa hao hadi Februari 13 mwaka huu kwa madai kwamba upelelezi juu ya shauri lao bado haujakamilika.
Watuhumiwa hao 61 wanakabiliwa na kesi ya kujihusisha na vitendo mbalimbali vya kigaidi ambapo kati ya hao watuhumiwa 23 wanatuhumiwa kwa kesi ya ugaidi nyumbani kwa Sheikh Sudy Ally Sudi julai 13 mwaka 2014.
Watuhumiwa hao wanatuhumiwa kufanya njama ya kufanya vitendo vya kigaidi nyumbani kwa Sheikh Sudi Julai 3, 2014 wakituhumiwa kurusha bomu la mkono na kumjeruhi kiongozi huyo huku baadhi yao wakituhumiwa kutoa msaada wa fedha kufadhili mpango huo.
Watuhumiwa wengine 13 wanatuhumiwa kufanya mauaji na kujaribu kuua ambapo kati ya mwaka 2014 watuhumiwa hao waliwaua Judith Mushi, Ramadhan Juma ,Fahad Jamal na Amir Daffa katika uwanja wa Soweto jijini Arusha.
Watuhumiwa 10 wanatuhumiwa kukusanya zana, kukutwa na zana na kusambaza zana yakiwemo mabomu mawili kati ya Julai 22 na 23 mwaka 2015 kwa lengo la kufanya ugaidi.
Watuhumiwa wanne kati ya 61 wanatuhumiwa kwa kosa la ugaidi ambapo kati ya Julai 2009 na Julai 2013 katika eneo la msikiti mkuu wa Arusha wanadaiwa kumwagia tindikali Mustapha Kiago na kumsababishia majeraha mwilini.
Watuhumiwa wengine wanne wanatuhumiwa kufanya vitendo vya ugaidi kati ya oktoba mosi na 25 mwaka 2012 nyumbani kwa Sheikh Abdulkarim Njonjo ambapo wanatuhumiwa kutupa bomu la kienyeji lililomjeruhi Sheikh Njonjo na kumsababishia majereha mwilini.
Watuhumiwa wengine watatu katika kesi hizo wanatuhumiwa kati ya machi 8 na julai 14 mwaka 2014 waliwashawishi vijana kujiunga na kikundi cha kigaidi cha Al-Shabaab.
Post A Comment: