Walimu wametakiwa kuwa na nidhamu katika kutekeleza majukumu yao kwa kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha  wanajituma  katika kufundisha pamoja na uwajibikaji uliotukuka ili kufikia malengo ya kupandisha kiwango cha taaluma katika halmashauri ya Arusha.

    Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Arusha Dkt. Wilson Mahera wakati akizungumza na walimu wa shule 25 za kata 9 za Ilboru, Moivo, Kiranyi, Ilkiding'a, Kimyaki, Olturoto, Sambasha, Mwandet na Olturumet kwenye ukumbi wa shule ya Sekondari ya Ilboru.

Mkurugenzi huyo amepata fursa ya kusikiliza kero, maoni na ushauri kutoka kwa walimu hao na kufanikiwa kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali na kuahidi kuendelea kutatua kero zote za walimu na kuwawezesha walimu kufanya kazi kwenye mazingira bora.

    Amewataka Walimu Wakuu kukaa na walimu na kufanya mikutano na kujadili maendeleo ya shule pamoja na kuwasikiliza walimu na kutatua changamoto za kiutumishi zinazowakabili  na kufanya kazi kwa pamoja kama timu kwa kuzingatia  sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

     Hata hivyo Dkt. Mahera amewataka walimu kuwa wazalendo  na zaidi  na kuwa na nidhamu katika utendaji na kuacha tabia ya kulalamika na kuwa na visingizio visivyo vya msingi katika utumishi wa umma.

    Ameongeza kuwa kuna baadhi ya walimu wasio na nidhamu na kuwa wasumbufu wasiokubaliana na kanuni na taratibu za utumishi  jambo ambalo linalosababisha walimu wengine kushindwa kuhudumiwa pale wanapokuwa na shida za kweli.

    "Kuna baadhi ya walimu ni wasumbufu mno, wamekuwa watoro, wavivu hawataki kufundisha na  kila wanachoelezwa hawataki kukubaliana na kutaka kufanyiwa kile wanachokitaka wao, walimu acheni tabia ya kujipangia majibu pale mnapohitaji kuhudumiwa.

Tunataka kupunguza kero za walimu kuanzia shuleni, walimu wakuu shughulikieni changamoto ndogo ndogo za walimu na muishi kama familia katika utendaji ila msiwaonee aibu walimu wasumbufu wajadilini kwenye vikao vyenu na kuleta taarifa zao kwenye ofisi yaMkurugenzi" amesisitiza Dkt. Mahera

Dkt. Mahera amethibitisha kuwa serikali ya awamu ya tano imejipanga kutatua changamoto za walimu kwa kuanza kulipa madeni ya walimu na kuongeza kuwa  halmashauri imeandaa mkakati wa kutafuta mwekezaji wa kujenga nyumba za walimu ambazo walimu watalazimika kulipia kiadi kidogo cha kodi kama ilivyo kwa watumishi wa mashirika mengine.

Ameongeza kuwa halmashauri inakabiliwa na changamoto ya nyumba za walimu na tatizo kubwa lipo kwenye shule zilizopo maeneo ya pembezoni ambako hakuna hata nyumba za kupangisha na kusababisha walimu kuishi mbali na eneo la shule. 

Aidha Dkt Mahera amesema kuwa halmashauri inakabiliwa na upungufu wa nyumba 2,583 ikiwa nyumba 1,643 kwa shule za msingi na nyumba 940 kwa walimu wa shule za sekondari.

Afisa Utumishi halmashauri ya Arusha Selemani Sekiete ametoa ufafanuzi kwa walimu juu ya stahiki za walimu kwenye likizo, ruhusa, uhamisho, kupanda daraja pamoja namna ya kubadilisha mahali pa kuzaliwa ikiwa mwalimu ameolewa.

Aidha Sekiete amewataka walimu kutambua kuwa kuna uhamisho wa kawaida ambao kisheri mtumishi anatakiwa kubadilishiwa kituo cha kazi kila baada ya miaka mitatu na kuwataka walimu kufahamu kuwa uhamisho huo sio adhabu ni uhamisho wa kawaida.

  1. Akizungumza kwa niaba  ya walimu hao  Afisa Elimu kata ya Moivo mwalimu Evaline Moshi amemshukuru Mkurugenzi na uongozi mzima kupata nafasi ya kuzungumza  na  walimu na kuwapa mikakati ya halmashauri pamoja na kufahamu dira ya halmashauri.


Ameongeza kuwa inatia moyo kiongozi anapokaa na watumishi kupanga mikakati ya pamoja na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa kwa lengo  kuhakikisha kupandisha kiwango cha taaluma pamoja na kuongeza ufaulu katika shule zote.

PICHA ZA MATUKIO YA KIKAO CHA WALIMU WA SHULE 25 NA KATA 9.

Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha Dkt. Wilson Mahera (aliyesimama) akizungumza na walimu kwenye Ukumbi wa Shule ya Sekondari Ilboru.





  

Walimu wakifuatilia hotuba ya Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha aliyoitoa kwa walimu.












Afisa Utumishi halmashauri ya Arusha Selemani Sekiete akitoa ufafanuzi juu ya haki, wajibu na stahiki za walimu wakati mkutano wa walimu na mkurugenzi wa halmashauri hiyo uliofanyika kwenye ukumbi wa shule ya sekondari Ilboru.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: