Viongozi 18 wa chama cha ACT-Wazalendo kutoka mikoa mbalimbali nchini wamejivua nyadhifa zao na kujiunga na CCM.
Viongozi hao wamepokelewa leo Januari 17, 2018 mjini Moshi na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira ambaye hivi karibuni alihamia chama tawala. Mghwira amewahi kuwa mwenyekiti wa ACT.
Miongoni mwa wanachama hao, wapo waliokuwa wajumbe wa kamati kuu, wenyeviti wa mikoa na makatibu wa ACT.
Pia, viongozi 18 wa Chadema ngazi za kata na vijiji kutoka Wilaya ya Siha nao wamejiunga na CCM.
Akizungumzia baada ya kuwakaribisha, Polepole amesema katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano, CCM kimeongeza wanachama zaidi ya milioni mbili.
"Tukisimamia haki na heshima kwa watu wote CCM kitatawala milele nchi hii. Kwa sababu misingi ya chama hiki ni utu. Sasa tunahitaji watu ambao wanachukizwa na rushwa, ubadhirifu na ubinafsi,” amesema Polepole.
Kwa upande wake Mghwira amesema siasa bado ina changamoto kubwa na kuwataka wanasiasa kufanya siasa za kuwaunganisha watu pamoja, si kujenga uadui.
"Nchi haiwezi kujengwa kwa maneno ya kashfa…,ili tupige hatua kimaendeleo inatakiwa  idadi ya vyama vya siasa ipungue kwa sababu utitiri  wa chama ni mkubwa ikilinganishwa na ukubwa wa nchi yete,” amesema Mghwira.
Aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT, Kansa Mbaruku amesema wamechukua maamuzi hayo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ya viongozi waandamizi wa chama hicho kuhama, akiwemo Mghwira .
Baadhi ya viongozi  hao ni Eva Kaka (mjumbe  Kamati Kuu),  mwenyekiti wa Mkoa wa Dodoma Anganile Massawe, Athuman Balozi (mwenyekiti mkoa wa Tabora), Hamad Nkya (mwenyekiti mkoa wa Kilimanjaro), Godwin Kayoka (katibu wa mkoa Tabora) na Juma Hamisi (mwenyekiti wazee mkoa wa Singida).
Share To:

msumbanews

Post A Comment: