NAIROBI: Hali ya wasiwasi imetanda nchini Kenya baada ya kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo Bwana Raila Odinga, kushikilia kuwa ataapishwa leo kama rais wa nchi hiyo.
Muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa) umesema hafla hiyo itafanyika katika uwanja wa Uhuru Park, Nairobi.
Baada ya sherehe hizo kuahirishwa mwezi uliopita, muungano mkuu wa upinzani nchini humo-NASA, bado unaendelea na msimamo wake wa kuwaapisha viongozi wake Raila Odinga na Stephen Kalonzo Musyoka, kama Rais na Makamu wa rais wa Jamhuri ya Kenya.
Maafisa wa polisi walifika asubuhi na mapema katika uwanja wa Uhuru Park, Nairobi unaopanga kutumiwa na muungano wa Nasa kwa shughuli ya kumuapisha Bw Odinga.
Mwandishi wa BBC David Wafula alipiga picha hizi za polisi wakiwa na magari maalum ya kukabiliana na ghasia wakishika doria uwanjani humo asubuhi na mapema.
Kituo cha habari cha kibinafsi cha Citizen kimeripoti kuwa maafisa wa polisi wameamrishwa kuondoka katika uwanja wa Uhuru Park.
Mabasi ya wafuasi wa upinzani yazuiwa Voi
Mabasi matatu yaliyokuwa yanawasafirisha wafuasi wa upinzani waliokuwa wanaelekea Nairobi kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwa kiongozi wao Raila Odinga yamekamatwa na maafisa wa polisi katika mji wa Voi, katika barabara ya kutoka Mombasa kwenda Nairobi.
Mji wa Voi unapatikana takriban kilomita 330 mashariki mwa mji huo mkuu wa Kenya.
Afisa wa polisi amewaambia wanahabari kwamba madereva wa mabasi hayo walikuwa wamevunja sheria kadha za barabarani.
Wafuasi wa upinzani waanza kuingia Uhuru Park
Wafuasi wa upinzani nchini Kenya wameanza kuingia uwanja wa Uhuru Park baada ya polisi kuondoka.
Baadhi wanazunguka uwanja huo wakiimba ‘Uhuru Must Go’.
Hali ilivyo uwanjani Uhuru Park
Mwandishi wetu David Wafula yupo uwanja wa Uhuru Park ambapo upinzani umepanga kumuapisha Raila Odinga kuwa kiongozi wa Kenya baadaye leo.
Wafuasi wa upinzani waliozuiliwa Voi waachiliwa
Wafuasi wa upinzani waliokuwa wanasafiri kuelekea Nairobi ambao walizuiliwa awali mjini Voi wameachiliwa na kuruhusiwa kuendelea na safari.
Post A Comment: