Kwa baadhi ya watu, hasa wanaume ambao wanaishi wenyewe (kuna wanawake pia wanaofanya hivyo) husahau ama huacha makusudi kufua shuka au mashuka wanayotumia kitandani hadi wakati mwingine yanaanza kutoa harufu mbaya na kukupa wakati mgumu kama umelala kitandani hapo.
Kufua shuka kwa baadhi ya watu si kazi rahisi kama kufua shati, hii i kutokana na ukubwa wake au kwa baadhi ya watu linakuwa limechafuka sana. Lakini suala la msingi ni kwamba, wataalamu wanashauri kwamba, shuka la kitandani linatakiwa kufuliwa ama kubadilishwa mara kwa mara.
Ili kuhakikisha kitanda chako hakiwi bustani ya kutunza fangasi na bakteria wa aina mbalimbali, mtaalamu wa masuala ya bailojia, Philip Tierno kutoka Chuo Kikuu cha New York, ameshauri kuwa, shuka linapaswa kufuliwa angalau mara moja kila wiki.
Unaweza ukasema kwamba, kwa wiki moja shuka lako halitakuwa limechafuka, lakini ujue kwamba, wakati umelala, mwili wako hutoa unyenyevu ama jasho ambalo hupelekea shuka kuchafuka na linaweza kukuletea bakteria ama fangasi endapo utakuwa hulifui mara kwa mara.
Shuka linaweza kuhifadhi uchafu wa aina mbalimbali kama vile vumbi, uchafu kutoka kwenye mimea ambayo inaweza kuwa hatari kwa afya ya ngozi yako. Lakini pia, mto unaotumia kitandani unaweza kutumika kuhifadhi hadi aina 16 za fangasi.
Kama unaona kuosha shuka mara moja kila wiki ni kazi ngumu, haupo peke yako. Wengi walioshiriki katika utafiti huu walieleza kwamba hufua mashuka siku 10 hadi 14 tangu waanze kuyatumia, wakati wengine walisema huyatumia hadi wiki tatu au nne kabla ya kufua.
Licha ya utofauti huo, kufua mara moja kila wiki ndio pendekezo la wataalamu. Na pia, unapofua unatakiwa kutumia maji ya moto (kwa mashuka ambayo yanaruhusiwa) ili kuua bakteria na fangasi wanaoweza kuwa wametengeneza makazi kwenye shuka lako.
Watu wengine huamka asubuhi wakiwa na mafua au maumivu katika koo, na hujiuliza bila kupata majibu kwamba wapi yote hayo yametokea, lakini ukweli ni kwamba, ni uchafu uliopo katika shuka lako.
Post A Comment: