Azory Gwanda 

Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari nchini (UTPC), umeiomba Serikali kuhakikisha mwandishi wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Azory Gwanda anapatikana.
Azory alichukuliwa na watu wanne waliokuwa kwenye gari jeupe aina ya Toyota Land Cruiser, Novemba 21,2017  katika mji wa Kibiti mkoani Pwani alikokuwa anaishi na kufanya kazi.

Mkurugenzi wa umoja huo, Abubakar Karsin ametoa kauli hiyo leo Jumatano Januari 24,2018 wakati wa mahojiano na mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe katika kipindi cha tujadiliane kinachoandaliwa na umoja huo na kurushwa na vyombo mbalimbali vya habari.

“Mwanzoni walianza kupotea watu wa kada zingine sasa imefika kwa waandishi wa habari. Hatujui zamu ya nani inafuata,” amesema Karsan.

Amesema hofu ya kuminywa kwa uhuru wa habari na maoni ulioikumba sekta ya habari nchini usipodhibitiwa utaunyima umma fursa ya kupata habari, hivyo kupunguza uwezo wa wananchi kushiriki, kujadili na kuamua masuala yanayowahusu.
Amebainisha kuwa, sekta ya habari nchini bado ina kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel ten, Daud Mwangosi aliyeuawa mikononi mwa polisi.

Karsan amesema kupotea kwa Azory kunatia chumvi maumivu ya wanahabari.
Kuhusu ukusanyaji wa habari, Karsan amemwomba Zitto kuwasilisha ombi la wanahabari kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ili awaeleze makamanda wa polisi wa mikoa kuondoa urasimu wa utoaji habari zinazohusu matukio ya jinai na uhalifu.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: