YANGA iliamua kuvunja benki na kufunga safari hadi Swaziland ili kuinasa saini ya kiungo, Papy Kabamba Tshishimbi aliyekuwa akiichezea Mbabane Swallows.
Pendekezo lilifanywa na Kocha Mzambia, George Lwandamina.
Kiu yao ilikuwa ni kutaka kuifanya Yanga iwe imara katika eneo la kati baada ya viungo waliosajiliwa tangu alipoondoka Mbuyu Twite kushindwa kuimudu vema.
Tshishimbi alipotua alitegemewa kutengeneza  pacha moja na Thabani Kamusoko aliyekuwa hana mtu wa kumsaidia katika eneo hilo, hata hivyo wawili hao walicheza kwa muda mfupi kabla ya Mzimbabwe kupata majeraha yaliyomuweka nje.
Tangu Kamusoko awe nje karibu miezi mitatu sasa, benchi la ufundi limekuwa likisaka pacha wa Tshishimbi kwa kutesti viungo kadhaa waliopo kikosini bila mafanikio.
Kabla ya kuumia Kamusoko alionekana kwenda sawa na Tshishimbi kwa kukaa, kutawanya mipira na kupiga mashuti mbali na pasi za mwisho, jukumu liliachwa kwa Rafael Daud, kisha Pato Ngonyani, lakini wawili hao walishindwa kwenda sawa na rasta huyo.
Wengine waliojaribiwa kucheza na Tshishimbi ni Pius Buswita, Said Juma ‘Makapu’ na huku chipukizi Maka Edward akipotezewa kwa kukosa uzoefu jambo alikuwa akicheza mechi kadhaa wakati mwingine kumpokea Mkongomani huyo.
Angalau kidogo Rafael alirandana na Mkongo huyo, lakini bado hakukuwa na ladha kama ile ya Kamusoko na Tshishimbi.
Katika mechi 14 ambazo Yanga imecheza mpaka sasa katika Ligi Kuu Bara, Mkongo huyo amekuwa akijaribiwa na viungo  tofauti, lakini ni wazi bado anamtesa Mzambia kwani hajapata pacha wake halisi kama tarajio la wengi.
Ilianza mechi yao na Lipuli ya 1-1 ambapo Tshishimbi na Kamusoko walipiga shoo ya nguvu. Ikaja dhidi ya Njombe Mji, wawili hao walicheza vema na Yanga kushinda bao 1-0 kisha ikaja mechi ya Majimaji hapo Kamusoko akaanza kukosekana na Tshishimbi alipewa Rafael na kushindwa kufanya vema licha ya sare ya 1-1.
Mechi yao ya Ndanda, Kamusoko akarudi na kuungana na Mkongo na mambo yakawa safi wakishinda 1-0.
Baadaye Yanga ikaifuata Kagera na Tshishimbi akapewa Makapu na matokeo yakaisha kwa ushindi wa 2-1, Yanga wakiibuka wababe, kisha wakasogea Shinyanga na Tshishimbi akapewa Rafael na Buswita na mechi ikaisha kwa Yanga kulala 1-0. Hata hivyo watatu hao walionekana kuiva licha ya kipigo hicho na ndio waliocheza pia dhidi ya Simba na mechi kuisha 1-1.
Viungo hao tena wakaenda Mwanza kucheza na Mbao na matokeo yakawa Yanga ikalala 2-0 huku viungo hao wakipoteana.
Mechi dhidi ya Prisons na Mwadui, Tshishimbi hakucheza na zikaisha kwa sare ya 1-1 na nyingine suluhu kabla ya juzi kati kurudi katika mechi dhidi ya Ruvu akipagwa na Makapu na kushindwa kuelewana.
Katika mechi za Kombe la Mapinduzi Yanga iliyotolewa nusu fainali, pia Tshishimbi alicheza mechi kadhaa akibadilishwa pia viungo wa kucheza nao na Kocha Msaidizi, Shadrack Nsajigwa alikiri wazi kukosekana kwa Kamusoko aliyeanza mazoezi kwa sasa ni pengo katika eneo la kati la timu yao.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: