Shirika la Fedha Duniani (IMF) limetahadharisha kwamba, ukuaji wa uchumi wa Tanzania unaweza kukumbwa na changamoto kutokana na hofu ya wawekezaji juu ya sera zisizotabirika.
IMF imesema kuwa, licha ya takwimu za pato la taifa kuendelea kukua, takwimu nyingine zinatahadharisha kuhusu kusinyaa kwa ukuaji wa uchumi.
Kuna hatari ya ukuaji mdogo wa uchumi kutokana na utekelezaji hafifu wa bajeti, uwepo wa changamoto nyingi katika mazingira ya biashara, na wasiwasi wa wawekezaji kuhusu utekelezaji wa sheria na sera, IMF imeeleza.
Hii imejidhihirisha katika kupungua kwa makusanyo ya mapato, kukwama kwa utaoaji wa mikopo ambapo kunashuhudiwakwa kuongezeka kwa mikopo chechefu katika benki za kibiashara.
Tanzania imekuwa na uchumi unaokua zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki ambapo umekua kwa 7.7% katika nusu ya kwanza ya mwaka 2017 ukilinganisha na Kenya mbao ulikua kwa 4.9% na Uganda 4.7%.
Makadirio yanaonyesha kuwa, kwa mwaka 2017 uchumi wa Tanzania ulikuwa kwa asilimia 7 ukilinganisha na Kenya uliokua kwa asilimia 5 na Uganda asilimia 5.1.
Aidha, IMF imeonya kuwa, sintofahamu iliyopo katika sekta ya uwekezaji na sekta binafsi kwa ujumla nchini Tanzania kutokana na sera za serikali, kunatishia ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Katika kipindi cha miaka miwili iyopita, serikali ya awamu ya tano imefanya mabadiliko mbalimbali ya sheria pamoja na sera ambazo zimesababisha kuyumba kwa uwekezaji hasa katika sekta ya madini.
Baadhi ya mabadiliko yaliyofanyika, hasa katika kodi yamepelekea baadhi ya kampuni zilizowekeza katika sekta ya madini kupunguza shughuli za uzalishaji nchini. Lakini wakati huo huo, serikali imekuwa ikijidhatiti katika ukusanyaji wa mapato ili kuwekeza kufadhili miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu.
Ulazima wa serikali kuongeza makusanyo ya mapato umeongezaka kwa sababu ya kupungua kwa vyanzo vingine vya mapato kama misaada kutoka nje, na wakati huo huo ukopaji katika benki za kibiashara umebaki njia panda, kwa mujibu wa Benki ya Dunia.
Post A Comment: