Baraza  la Vyama vya Siasa limeunda kamati tano na kuzipa mwezi mmoja kupitia mapendekezo ya Sheria mpya ya Vyama vya Siasa na Kanuni za usajili wa vyama.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Baraza hilo, John Shibuda alisema kamati hizo zitafanya mapitio ya mapendekezo ya sheria mpya na kanuni ndani ya wiki mbili ili kuona usahihi wa vifungu vilivyopo.

Alisema baada ya mapitio hayo kamati hizo zinatakiwa zikamilishe maboresho ndani ya mwezi mmoja.

“Baraza limezipa wiki mbili kamati ili ziweze kujipanga na kupitia mchakato halafu ndani ya mwezi mmoja waweze kukamilisha na kutoa taarifa za kutosha,” alisema Shibuda.

Alisema baada ya maboresho kukamilishwa watatoa mapendekezo kwa mwenyekiti ambaye ataitisha kikao na kuyajadili kisha itaandaliwa rasimu.

Shibuda alisema, hadi sasa mchakato wa kutunga sheria na kanuni za usajili wa vyama vya siasa bado haujatekelezwa na badala yake zimeunda kamati ambazo zitachakata mapendekezo.

“Hadi sasa tunaendelea na sheria na kanuni zilezile za usajili wa vyama vya siasa, mapendekezo yaliyokuja kutoka sekretarieti yanaenda kuchakatwa na kamati ya sheria na Utawala Bora ya baraza,” alisema Shibuda.

Alisema baraza ndilo litakaloridhia yapi yanafaa kuwa mapendekezo ya vyama vya siasa kwa ajili ya kutungwa kwa sheria.

Shibuda alisema baraza hilo lipo huru na vyama vyote vimeshiriki wakiwamo wajumbe kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao wamewakilishwa na Salum Mwalimu ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar (Chadema) na wajumbe wengine kutoka vyama mbalimbali.

Amezitaja kamati zilizoteuliwa na viongozi wake ni Kamati ya Bunge na Siasa, Mwenyekiti Juju Martini Danda (NCCR-Mageuzi) na Makamu Mwenyekiti ni Mohamed Masoud Rashid (Chauma).

Nyingine ni kamati ya Sheria na Utawala Bora ambapo mwenyekiti wake ni Hassan Almas (NRA) na Makamu wake ni Said Sudi.

Shibuda aliitaja pia Kamati ya Maadili na Mahusiano inayoongozwa na Mohamed Ally Abdallah (Demokrasia Makini) na Peter Magwira (Democratic Party).

Kamati ya fedha Mwenyekiti John Cheyo (UDP) na Salum Mwalimu ambapo ile ya Uongozi wa Baraza la vyama vya Siasa, Shibuda na Dk. Abdallah Juma Saadala.

Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC),  Doyo Hassan alisema hajaona sababu za mapendekezo hayo kuundiwa kamati.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: