Unaweza kujiuliza kwa nini wanawake watu wazima wanataka wanaume waliowazidi umri.
Ipo mifano mingi katika jamii yetu wakiwamo watu maarufu, viongozi na wasanii ambao wapo katika uhusiano wa kimapenzi au ndoa na wanaume waliwazidi umri.
Mahojiano mafupi yaliyofanywa na gazeti hili kwa baadhi ya watu yamepata sababu kadhaa zinazoweza kuwa jibu la swali hilo.
Miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na wanaume wenye umri sawa na wanawake hao hawana mvuto tena.
Baadhi ya wanawake waliohojiwa walisema kuwa wanaona haya kuwa na wanaume waliowazidi umri, ingawa huvutiwa nao.
“Kwa kweli wanaume walio na umri mdogo wanavutia, hasa umkute aliyejengeka vema, ila kuwa naye kunahitaji moyo wa chuma hasa ka sisi ambao tumeshazaa.
Imelda anaeleza mapenzi hayana umri, jamii hasa ya sasa ndiyo imechanganya umri na mapenzi. Anazitaja sababu zinazowachosha wanawake watu wazima kuwa na wanaume wa umri wao ni sawa na kuwa na gari bovu kusukumwa na bovu.
“Unajua ikifika mahali fulani, wanaume anakuwa hawana mikikimikiki furaha, kibaya au kizuri wanawake wakifika umri wa utu uzima ndiyo wanafurahia zaidi faragha.
“Hivyo ukiwa na mtu mzima mwenzako bila shaka hautapata unachokitaka, ndiyo maana wengi tunatamani kuwa na vijana ambao wanamudu mambo hayo, ”anasema Imelda.
Imelda anatoa takwimu kwa upande wake kuwa kati ya wanawake watu wazima 10 ni watano pekee ambao hupenda kuwa na wanaume wa umri wao.
Anasema wanawake hasa watu wazima mara nyingi hawapendi kuwa chini ya mwingine, hususani linapokuja suala la kujamiiana, hivyo wakiwa na vijana hupata fursa ya kutawala uhusiano wao ndani na nje.
Hoja ya Siwema inaungwa mkono na Fadhili Idrissa anayesema kuwa: “Mimi pia ninapenda kuwa na mwanamke aliyenizidi umri kwa sababu ninaamini atanipa ninachotaka ikiwamo kutawala mchezo tukiwa faragha.
“Hawa wasichana au wanawake wa rika langu wanataka kubembelezwa na zaidi kupenda mapenzi ya kuiga, wanawake waliotuzidi umri hawana cha urembo wala majivuno, wao hutumia akili kuhakikisha penzi lao haliingiliwi na vijana, ndiyo maana wanakuwa makini,” anasema Idrissa.
Fadhili anafafanua kuwa ni kazi kulinda penzi la msichana au mwanamke mwenye umri mdogo kuliko mwanaume kwa sababu ya vitu vingi ikiwamo tofauti ya mihemko yao.
Anasema wanawake wengi wakiwa na umri mdogo kuna vitu wanapenda ambavyo kwa mwanaume ama vinakuwa ni anasa, gharama kubwa au usumbufu.
Anasema kikubwa wanachonufaika ni uzoefu wa uhusiano wanaokuwa nao kina mama hao, jambo linalofanya mapenzi yawe ya furaha.
“Mwanamke ukimpa nafasi anafanya zaidi ya ulivyokusudia, sasa akishakuwa mkubwa, inakuwa rahisi hata kumaliza tofauti zenu kwa sababu anatambua jukumu la kulinda uhusiano huo ni lake kutokana na kuwa na umri mkubwa.
“Nakuambia akiwa hivyo hakusumbui, anajua yeye ndiyo kichwa, anajua anatakiwa kuongoza jahazi hilo, huku akiamini kushindwa na kijana mdogo ni ni aibu hivyo atafanya kila analoweza kuhakikisha mnakwenda sawa, ” anasema Idrissa.
Sababu nyingine tofauti na hizo inatolewa na Mwamvua Hamisi anayesema kuwa vijana wadogo ndiyo rahisi kuwamiliki kuliko watu wazima.
Anasema kwa mfano mwanamke aliyefiwa au kuachwa na mwenza wake, siyo rahisi kumpata mwanaume wa rika lake ambaye hajaoa.
“Ili upate kitu chako mwenyewe na ambacho utakimiliki, lazima atakuwa kijana mdogo ili kuepuka kuingilia uhusiano wa watu.
“Vijana kuna vitu vinawakera na unavikosa, penzi la dhati, kupigwa mizinga, kulaumiwa, hivyo akija kwako unahakikisha karaha ndogo ndogo hana. “Unampiga pamba, kama kasoma unapambana apate kazi nzuri au unamfungulia biashara hapo utakuwa umemilikia, ingawa itakubidi ubadili mtizamo kutoka wa miaka 40-50 kuja wa miaka 20-25 ikiwamo uvaaji, utembeaji, kuzungumza na hata marafiki,”anasema Mwamvua.
Mamvua anafafanua iwapo kuwa na kijana ni faraja kwa muhusika haoni kama kuna ugumu, ugumu unaletwa na wapambe wa pembeni wanaochanganya umri na matakwa ya moyo.
Anasema mwanamke mtu mzima anapokuwa na kijana hujihisi na yeye ni msichana, hivyo huleta faraja maishani.
“Mapenzi, vichekesho, utoto mwingi, mavazi, maeneo ya mitoko humfanya ajione binti wa miaka 20. Naye Phidelis Michael anasema mwanamke mtu mzima akiwa na kijana hujifunza vitu vingi vipya.
Anasema atalazimika kuishi maisha ya ujana na kujikuta akifuatilia kinachoendelea mitandaoni, kwenye vyombo vya habari, vitabuni, tamthilia na hata vilivyomo ndani ya simu yake ya mkononi. “Unadhani mwanamke aliye ndani ya ndoa ambaye siyo msomi, mwenye miaka zaidi ya 40 atahangaika na hayo mambo, lakini akiwa na kijana aliyemzidi umri bila shaka ataiga mambo anayoyafanya na kujikuta yupo kidigitali zaidi, ”anasema Michael.
Kwa upande wa Husna Maulid anasema kwake kuwa na kijana mwenye umri mdogo siyo heshima na haoni sababu yoyote ya maana kwa mwanamke mtu mzima kujitetea kwa hilo.
Anasema inajulikana tangu enzi mtu mzima hususani mwanamke amkanye kijana akikosea, sasa kwa utaratibu wa kuwa na uhusiano nao heshima inakuwa hakuna.
“Ndiyo maana vijana wa siku hizi wa kike na kiume hawana adabu, hii inatokana na kutokuwa na mipaka kati yao, kama unaweza kutoka kimapenzi na kijana uliyemzidi zaidi ya miaka 10 kwa visingizio hivi na vile unadhani kuna nafasi ya heshima hapo” anasema na kuhoji Husna.
Anasema hii imetokana na binadamu kupenda kufanya vitu vinavyokatazwa na kutamani kuona itakuwaje.
Wataalamu wa saikolojia wafafanua
Mtaalamu wa saikolojia ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini kutokana na majukumu mengine aliyonayo, anasema hali hiyo hutokana na binadamu kupenda vitu vipya.
Anasema linapokuja suala la kujamiiana, wanawake wanapokuwa watu wazima baadhi yao huwa hawana hamu kama vijana, “Hivyo wanaamini wakipata mwanaume mwenye umri mdogo kuliko wao husisimua hisia zao. Naye mtaalamu wa saikolojia kutoka katika Chuo Cha ualimu Patandi tawi la Sahare Tanga, Modester Kimonga anasema binadamu huwa ana balehe mbili.
Anasema ya kwanza ni ile ya umri kati ya miaka 14 na kuendelee kwa wavulana na miaka tisa na kuendelea kwa wasichana.
Anaitaja balehe ya pili ni anapofikisha umri wa miaka kati ya 35 na 40, msukumo wa balehe hii ni kutamani kufanya mambo aliyokuwa akifanya akiwa mvulana au msichana. Anasema kwa wanawake hupenda kufanyiwa mambo waliyokuwa wanafanyiwa wakiwa wasichana wabichi, miongoni mwa mambo hayo ambayo huyapenda kisaikolojia ni pamoja na kusifiwa.
“Hilo husababisha waone bora kuwa na wanaume waliowazidi umri ili wawasifie hata kwa mambo ya kawaida, ndiyo maana wakishaingia katika mahusiano hayo hubadilika kila kitu ikiwamo mavazi na kujiona ni vijana, ”anasema Kimonga.
Kimonga anaongeza kuwa pia wanawake kutokana na historia zao a utotoni baadhi yao walipata wanaume waliokuwa wanawadidimiza, hivyo kuwa na vijana hao kunawapa nguvu ya kutawala uhusiano wao.
Kwa upande wa mtaalamu wa saikolojia kutoka kituo cha Nehota Mental Health, Bonaventura Balige anasema anachofahamu kisaikolojia ni kawaida wanaume wakubwa kutaka wadogo kwa sababu wanaake wanakua haraka kuliko wanaume.
“Kwa mfano wanawake wenye umri sawa na mimi hivi sasa ni wakubwa, ninaweza hata kuwaamkia, na mwanaume hata akiwa katika uhusiano na binti aliyemzidi miaka 20 wanaweza kukaa pamoja wakajadili na hata akashauriwa.
“Hiyo ni tofauti kwa mwanamke kukaa na mwanaume aliyemzidi umri na akamshauri, ndiyo maana nashindwa kujibu moja kwa moja sababu zinazowafanya wanawake wakubwa kupenda vijana wadogo”anasema Balige.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: