JUMA NYOSO.

SIKU chache baada ya kuachiwa kwa dhamana beki wa kati wa Kagera Sugar, uongozi wa timu hiyo umetoa sababu kwa nini hawatamchukulia hatua mchezaji huyo anayetuhumiwa na madai ya kumpiga shabiki wa soka.

Nyoso, alikamatwa na Jeshi la Polisi mara baada ya mchezo wao wa ligi kuu dhidi ya Simba uliofanyika kwenye uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na wenyeji kulala kwa mabao 2-0.

Akizungumza jana na kituo kimoja cha redio, Mratibu wa Kagera Sugar, Mohamed Hussein, alisema kuwa klabu hiyo haitamchukulia hatua yoyote Nyoso kutokana na kitendo hicho kwa sababu jambo hilo lilifanyika nje ya uwanja na pia shabiki huyo Shabaan Hussein alimfanyia vitendo vya ‘kumpandisha hasira’ Nyoso.

“Nyoso kwa sasa yupo nje kwa dhamana na amejiunga na kambi ya timu, lakini niweke wazi hatotumchukulia hatua yoyote sisi kama klabu,” alisema Hussein.

Alisema kuwa Nyoso ni binadamu na kitendo cha shabiki yule kumpulizia Vuvuzela sikioni na kumtukana kilimtia hasira.

“Hatukubaliani na kitendo cha kupiga shabiki, lakini kama ni adhabu basi vyombo vya dola au Shirikisho (TFF),” aliongeza kusema.

Nyoso aliwekwa mahabusu kuanzia Jumatatu mpaka juzi baada ya hali ya shabiki huyo kuwa mbaya katika kipindi hicho.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: