HAKIMU Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Michael Mteite, jana aliamuru Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi 'Sugu' na katibu wa Chama hicho Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga, wapelekwe mahabusu katika kesi ya kutumia lugha za fedheha dhidi ya Rais Magufuli.

Hakimu Mteite alifikia uamuzi huo baada ya wakili wa serikali, Joseph Pande, kuomba wasipewe dhamana kwa usalama wa maisha yao baada ya kupandishwa kizimbani mahakamani hapo. Walipelekwa katika Gereza la Ruanda.

Mteite alisema uamuzi wa dhamana kwa washtakiwa hao atatoa keshokutwa.
Awali mbele ya mahakama, wakili wa serikali Pande alidai kuwa washtakiwa hao walitumia lugha za fedheha dhidi ya Rais John Magufuli Desemba 30, mwaka jana katika viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge.

Pande alisema upelelezi wa shauri hilo umekamilika na wapo tayari kuendelea kusikiliza kesi hiyo.
“Kosa walilolitenda washtakiwa ni kutoa maneno ya fedheha yanayomtaja Rais kuwa muuaji hivyo wakiwa nje wanaweza kupata matatizo kwa wananchi ambao hawajapendezwa na maneno hayo,” alidai wakili Pande.

Wakili wa utetezi Sabina Yongo aliomba muda kabla ya kuanza usikilizaji, hata hivyo, kwa kuwa shauri hilo ndiyo limefikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza.
Alisema anahitaji muda wa kukaa na 'Sugu' na Masonga ili kujadiliana nao juu ya shauri hilo, ikiwemo kupatiwa dhamana baada ya wakili Pande kuomba mahakama kutowapatia dhamana washtakiwa kwa madai ya kulinda usalama wao.

Washtakiwa hao wanadaiwa kufanya uchochezi kwa kutoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais Magufuli Desemba 30, mwaka jana ambapo Sugu anadaiwa kutamka kuwa Rais ni muuaji. 
Share To:

msumbanews

Post A Comment: