Mkuu wa Mkoa Manyara, Alexander Mnyeti


Serikali Mkoani Manyara imetoa mifuko 100 ya saruji kuunga mkono wakazi wa wa kijiji cha Ngage katika ujenzi wa kituo kipya cha polisi kinachotarajiwa kujengwa kwa nguvu za wananchi hivi karibuni.

Wakazi hao wameamua kujenga kituo hicho kama njia ya kukomesha mapigano ya mara kwa mara baina ya wakulima na wafungaji.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara kijijini hapa juzi, Mkuu wa Mkoa Manyara, Alexander Mnyeti alisema mifuko hiyo ya saruji imetolewa kufuatia maombi ya wanakijiji kutaka kujenga kituo hicho.

Alisema baada ya malalamiko ya wananchi kutaka kituo cha polisi ili uhalifu wa mapigano baina ya wakulima na wafugaji udhibitiwe, serikali ya mkoa imeona ni vema kuunga mkono juhudi za wananchi.
"Mmetoa maombi yenu ya kutaka kituo cha polisi mahali hapa, kilio chenu nimekisikia na ninachokitaka kwenu ni kuhakikisha mnatoa ushirikiano mkubwa katika ujenzi wa kituo hiki," alisema Mnyeti.

“Tafuteni kiwanja kwa ajili ya ujenzi na mimi nawaunga mkono kwa kuchangia mifuko 100 ya saruji na mtakapokuwa mmejenga kufikia lenta bati nitaleta."
Aidha alisema kazi ya serikali ni kuhakikisha amani inakuwepo kwa wananchi wake ili waweze kuendelea na shughuli za maendeleo, kwa kuwa bila amani hakuna maendeleo yoyote.

Aidha, Mnyeti alimtaka Mwenyekiti wa kijiji hicho, Korodun Lenjoro, kuhakikisha wananchi wanatoa ushirikiano wao wa dhati katika kuchangia mchango huo wa ujenzi wa kituo hicho.

"Mwenyekiti anza mpango wa uchangishaji wa michango ya ujenzi wa kituo hiki mara moja," alisema Mnyeti kwa kuwa "wewe na serikali yako mna jukumu la kutatua migogoro yenu". 
"Miingiliano ya maeneo ya mifugo na kilimo ni tatizo linalotakiwa kutatuliwa mara moja."
Alimtaka Mkuu wa Polisi (OCD) Wilaya ya Simanjiro, Juma Majata, kuwafikishia ramani itakayotumika katika ujenzi wa kituo hicho ndani ya siku mbili.

Pia alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula, kuhakikisha anatenga matumizi bora ya ardhi ili kuondokana na wakulima na wafugaji kuingiliana katika maeneo ya kilimo, ufugaji na makazi ya watu.
Mapema Mwenyekiti wa kijiji cha Ngage, Lenjoro, alisema ujio wa Mkuu wa Mkoa kijijini hapo umekuwa wa faraja kwao.

Alisema ujenzi wa kituo hicho utasaidia kuondokana na uhalifu mbalimbali.
Alisema awali walikuwa wakipata adha kubwa ya kufuata huduma ya kipolisi wilayani kwa kusafiri umbali wa kilomita 100.
Alisema kutokana na ongezeko la watu kijijini hapo linalosababishwa na kilimo cha vitunguu, ujenzi wa kituo cha polisi utasaidia kuleta amani na utulivu kwa wakazi wake.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: