Serikali imetoa muda wa miezi tisa kwa wafanyabiashara wa magari, kuhamishia biashara zao (Showroom) katika eneo la Kigamboni lililotengwa maalum kwa ajili ya biashara hiyo.

Akizungumza na wafanyabiashara hao leo, Jumatano, Januari 24, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema hakutakuwa na lugah nyingine ya kuongezewa muda indi miezi hiyo itakapokamilika.
“Tusije tukafika hatua, mwezi wa tisa tukaanza tena kuvutana, kupimana nguvu kuona.. Bahati mbaya kifua changu ni kikubwa, huwa hakiipimwi. Kwa hiyo niwaombeni tena, mmeomba wenyewe tuongeze muda na muda wa kwangu niliokuwa nimepanga kuongeza ni miezi sita, lakini tunakwenda mpaka miezi tisa kutokana na maombi ya kwenu,” amesema Paul Makonda.
Makonda amewahakikishia wafanyabiashara hao kuwa, ndani ya kipindi hicho cha miezi tisa, barabara, umeme wa uhakika, mfumo wa maji pamoja na kituo cha polisi kwa ajili ya ulinzi, vitakuwa vimekamilika kujengwa katika eneo hilo maalumu kwa ajili ya uuzwaji wa magari.
“Kwa upande wa kwetu na sisi tunaendelea kukimbisa mambo yaliyobaki kuhakikisha kwamba inapofika kipindi kile, atleast tumepunguza kwa kiwango kikubwa. Barabara nimewaahidi kwamba itapitika, lakini inaingia kwenye upande wa ujenzi wa lami mwaka huu, laini la maji natumaini litakwenda vizuri, la umeme sina wasiwasi nalo, limeshapiga hatua kubwa. Upande wa polisi ni kuanza ujenzi wa kituo chetu na mafundi tunao, wanajenga polisi wenyewe. Kwa hiyo nina imani na mimi kwa upande wangu nitakuwa nimeshapiga hatua nzuri kuhakikisha yale mazingira tumeyaboresha,” amesema Makonda.
Amesema kuwa taarifa za awali zimebainisha kuwa wafanyabiashara wengi ambao hawataki kuhamia kigamboni ni wale ambao wamekua wakitumia ujanja mwingi katika ufanyaji wa biashara zao, ikiwemo kuingiza magari mabovu pamoja na kuyatumia kupitisha dawa za kulevya.
“Ukimuona mwingine anahangaika kuvutavuta, jua hata magari yake mengi ni mabovu. Eidha alikuwa anakata mkanda,.. au huyu bwana alikuwa anachukua magari ya wizi, .. au mwingine yadi yake inaongoza kwa kukodisha magari lakini yako kwenye yadi, ana plate number maalumu watu wakikodi. Hayajalipiwa kitu chochote kile, hata kodi. Mwingine ndiyo hivyo, ukiona anabisha jua huyu alikuwa anafanya biashara ya madawa ya kulevya,”amesema.
Wafanyabiashara hao wameeleza kuridhishwa na muda ulioongezwa huku wakisifia uamuzi huo na kusema kuwa utawajengea imani na wateja wao kwani utawaepusha na matapeli ambao hujifanya wafanyabiashara wa magari.
“Kwa hiyo pia, hii kwa wateja watakuwa na uhakika. Ananunua kitu sehemu ambapo anajua sasa amenunua kitu ambacho  tunasema value for money. Katoa pesa lakini amepata product ambayo ni nzuri na sehemu ambayo anajua leo na kesho, nikitaka kwenda kuulizia au kubadilisha ile gari au kufanya jambo jingine lolote anapiga moto, anaenda Kigamboni,” amesema Mkurugenzi wa Chikasa, Salim Chikago.
Awali muda wa kuhamia kwa wafanyabiashara hao eneo la Kigamboni lenye ukubwa wa ‘square metre’ 750,000, ulitakiwa kuanza Januari mwaka huu, lakini kutokana na kutokukamilika kwa ujenzi wa miundombinu, pamoja na wafanyabiashara wengi kushindwa kuhamia eneo hilo, serikali imeongeza muda wa miezi 9 ili ifikapo mwezi wa Oktoba, wafanyabiashara wote wawe tayari wameshahamia katika eneo hilo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: