Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, amepiga marufuku utaratibu wa wananchi wa vijiji vitatu vya Remng’orori, Mikomarilo na Sirorisimba vilivyoko katika wilaya za Bunda, Serengeti na Butiama vinavyogambania mipaka ya wilaya zao, kupiga yowe pale inapotokea kuwapo na jambo la hatari.
Marufuku hiyo imekwenda sambamba na katazo la kuzuia shughuli zozote zikiwamo za kilimo eneo linalogombaniwa, kutotumiwa na pande zote hadi hapo Serikali itakapoamua vinginevyo, ikiwa ni njia pekee ya kuzuia athari zitakazoweza kutokea.
Malima amewataka wananchi wa vijiji hivyo kutoa taarifa Jeshi la Polisi pale linapotokea jambo la kiuhalifu au linalohatarisha usalama wao, kuliko kujichukulia sheria mkononi na kusababisha uvunjifu wa amani.
Malima alisema amelazimika kuzuia yowe katika vijiji hivyo kwa sababu amebaini ilikuwa ikitumika vibaya kwa kukusanya watu kwa hisia zisizo za kweli, huku baadhi ya wananchi wakitumia nafasi hiyo kufanya uchochezi dhidi ya upande mwingine.
“Kwanza nimezuia eneo lile linalogombaniwa maarufu ‘Sambusa’ lisitumiwe na pande zote, pia utaratibu wa kupiga yowe nimezuia kabisa hata kama kuna jambo lolote la hatari, wanachotakiwa kufanya ni kutoa taarifa polisi kwani wao ndio waliopewa jukumu la kulinda raia na mali zao.
“Nimefanya hivyo kwa sababu tangu kutokea tukio la uvamizi lililosababisha watu wawili kuuawa, sasa kila mtu akiona wakiwa wawili au watatu anaanza kuwa na hofu na kupiga yowe, ikiashiria kuomba msaada upande wa kijiji chake na watu kujikusanya, hapo ndipo uchochezi unapotokea kwa sababu ya hisia za mtu,” alisema.
Post A Comment: