Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Profesa James Mdoe amesema Taifa letu haliwezi kufikia malengo ya kuwa nchi ya Kipato cha Kati hadi itakapoweza kuwezesha watu kuwa na stadi za kazi ili waweze kuchangia maendeleo ya viwanda na uchumi kwa ujumla.
Prof. Mdoe amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kuhusu Uandishi wa Miradi ya Kuendeleza Stadi za Kazi, kwa waajiri na vyuo vya mafunzo kuanzia ngazi ya ufundi stadi hadi vyuo vikuu chini ya mradi wa kukiza stadi hizo (ESPJ).
Profesa Mdoe amewaambia Washiriki hao kuwa lengo la kuwepo Mradi wa ESPJ ni kufanya maboresho katika mifumo ya uboreshaji wa mafunzo ya stadi za kazi (Strengthening the institutional capacity of the skills development system) na kuongeza idadi na ubora wa wahitimu wa mafunzo ya stadi hizo kulingana na mahitaji ya soko la ajira katika sekta zenya kukua kwa haraka.
Prodesa Mdoe amesisitiza kuwa Wizara itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Sekta Binafsi ili kuviwezesha vyuo kuanzisha au kuboresha programu za mafunzo zinazoendana na mahitaji ya sekta binafsi.
Kwa upande wake mratibu wa Mradi wa Kukuza Stadi za Kazi (ESPJ) Dk. Jonathan Mbwambo, alisisitiza kuwa tofauti na utaratibu wa kuomba na kupangiwa fedha kwa ajili ya mafunzo, mfumo huu unawataka watoa mafunzo kuandika miradi ya kuendeleza stadi za kazi na kuziwasilisha serikalini ili kuchambuliwa na miradi itakayoshinda kupatiwa fedha.
Mafunzo hayo ya Siku mbili yalijumuisha washiriki 67 na yaliyoratibiwa na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na Benki kuu ya dunia.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
26/1/2018
Post A Comment: