Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro, amekagua nyumba za askari zilizoungua moto Septemba, mwaka jana ambazo kwa sasa zimefikia hatua za mwisho kukamilika.
Kuungua kwa nyumba hizo kulisababisha familia 13 za polisi kukosa mahali pa kuishi na kupoteza mali zao zote.
Katika ziara yake aliyoifanya mwishoni mwa wiki jijini hapa, IGP, Sirro alimshukuru Rais John Magufuli kwa kutoa Sh. milioni 260 za ujenzi wa nyumba hizo, ambazo hivi sasa zipo katika hatua ya mwisho kukamilika.
Aidha, IGP alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na kamati ya ulinzi ya mkoa kwa kuhamasisha wafanyabiashara wa mkoa huo, ambao kwa umoja wao walimuunga mkono Rais kwa kujenga nyumba 18.
IGP Sirro alitembelea pia ujenzi wa vituo viwili ya polisi - Muriet na kituo cha polisi maalum kwa ajili ya watalii vilivyojengwa kwa ufadhili wa wafanyabiashara hao.
Post A Comment: