Ofisa kilimo wa Kijiji cha Bukene Kata ya Didia Shinyanga Vijijini, Edward Ntogo (32), ameuwa na watu watano wanaosadikiwa ni majambazi.
Aliuawa kwa  kupigwa risasi kichwani kwenye paji la uso na kutokezea kisogoni na kupoteza maisha papo hapo.

Tukio hilo lilitokea juzi saa 2;40 usiku, wakati majambazi hao wakiwa kwenye kata hiyo wakifanya uharifu wa kupora mali kwenye maduka.
Wakati wakiendelea kufanya uhalifu huo, ndipo walipompiga risasi ya kichwa kwa kutumia bunduki aina ya SMG.

Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Simon Haule, alisema chanzo cha tukio hilo ni kuwania mali, ambapo majambazi hao awali walikutana na marehemu wakati wakienda kupora duka la mfanyabiashara Juma Mnyesi.

Alisema baada ya kumaliza kupora duka hilo walimjeruhi Mnyesi pamoja na mkewe Mariamu Mkubwa, na  kumpora  Sh. milioni 2 za mauzo, kisha kumrudia marehemu, ambaye katika harakati za kujikwamua walimpiga risasi na kufariki.

“Watu hao wanaosadikiwa ni majambazi  walikuwa na silaha za moto na mapanga, ambapo katika eneo la tukio ziliokotwa risasi mbili na maganda 11 ya SMG na baada ya kufanya matukio hayo walikimbilia kusikojulikana,” alisema Kamanda Haule.

Aliongeza mwili wa marehemu Ntogo umehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika Rospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga, na kwamba Mnyesi na mkewe Mariamu Mkubwa, wamelazwa katika Kituo cha Afya cha Bugisi Shinyanga Vijijini na hali zao zinaendelea vizuri. 
Share To:

msumbanews

Post A Comment: